SuperSport kurusha mechi zote 104 za Kombe la Dunia 2026 mubashara

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya matangazo ya michezo ya SuperSport chini ya DStv, kampuni tanzu ya MultiChoice Group na kampuni ya CANAL+ imetangaza rasmi kuwa itarusha mubashara mechi zote 104 za FIFA World Cup 2026, tukio linalotarajiwa kuweka historia mpya katika soka la dunia.
Taarifa hiyo iliyotolewa Aprili 17, 2026, inaeleza kuwa mashindano hayo yatakayofanyika katika nchi za Mexico, Canada na United States yataoneshwa kwa wateja wote wa DStv na DStv Stream, kuanzia kifurushi cha Access hadi Premium.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia, mechi zote zitapatikana kwa urahisi kwa watazamaji wengi zaidi barani Afrika, huku pia zikijumuisha vipindi vya uchambuzi, muhtasari na marudio ya michezo hiyo,” imesema taarifa.
Mashindano ya mwaka 2026 yatakuwa ya kipekee zaidi baada ya kupanuliwa kutoka timu 32 hadi 48, hatua itakayoongeza idadi ya mechi hadi 104. Michuano hiyo itaanza Juni 11, 2026 katika mji wa Mexico City na kufikia tamati Julai 19, 2026 kwa mchezo wa fainali utakaopigwa New Jersey.
Katika kuhakikisha uzinduzi wa matangazo hayo unapata mvuto wa kipekee, DStv ilishirikiana na staa wa Hollywood Idris Elba ambaye alitangaza rasmi kurushwa kwa mechi zote 104 mubashara kupitia jukwaa hilo.
Afrika yaandika historia
Kwa upande wa Afrika, bara hilo linatarajiwa kuandika historia kwa kupeleka timu 10 kwenye fainali za Kombe la Dunia, idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea. Mataifa hayo ni pamoja na Ghana, South Africa, Senegal, Cape Verde, Côte d’Ivoire, Egypt, Algeria, Morocco, Tunisia pamoja na Democratic Republic of the Congo.
Ushiriki huo mkubwa unatarajiwa kuongeza ladha ya kipekee ya soka la Afrika katika jukwaa la kimataifa, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona ushindani mkali kutoka kwa timu hizo.
Akizungumzia maandalizi hayo, Mkurugenzi wa Maudhui na Michezo wa CANAL+ kwa Afrika inayozungumza Kiingereza na Kireno, Rendani Ramovha, amesema kuwa wanajivunia kuwaletea Waafrika mashindano hayo makubwa kwa ubora wa hali ya juu.
Amesema upanuzi wa michuano hiyo pamoja na idadi kubwa ya timu za Afrika ni fursa muhimu kwa bara hilo kujionesha zaidi kimataifa, huku akisisitiza kuwa DStv imejipanga kuhakikisha wateja wanapata uzoefu bora wa utazamaji.
Mbali na matangazo ya moja kwa moja, SuperSport pia imeandaa vipindi maalum vya uchambuzi vitakavyoshirikisha wachambuzi wa ndani na kimataifa, pamoja na maudhui yatakayolenga tamaduni na lugha za Kiafrika.
Kwa ujumla, Kombe la Dunia la 2026 linatarajiwa kuwa la kihistoria si tu kwa ukubwa wake, bali pia kwa namna litakavyowafikia mashabiki wengi zaidi barani Afrika kupitia majukwaa ya kisasa ya matangazo



