Ligi Kuu

Pedro: Tulibadili mfumo kutokana na mazingira ya mchezo

 MWANZA: KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves, amesema walilazimika kubadili mfumo wa uchezaji katika mechi yao dhidi ya Pamba kutokana na tofauti ya mazingira ya mchezo, aina ya uwanja pamoja na hali ya mpinzani.

Akizungumza jijini Mwanza baada ya mchezo dhidi ya Pamba walioshinda mabao 3-0 Pedro amesema timu yake inaendelea kujengwa hatua kwa hatua, huku kila mazoezi yakitoa nafasi ya kuongeza mbinu mpya, ufumbuzi tofauti na sura mpya ya kiuchezaji kulingana na mahitaji ya kila mechi.

Amesema kuwa mechi hiyo ilikuwa na mazingira tofauti na michezo mingine, jambo lililowalazimu kuingia na mpangilio wa kiufundi uliokuwa tofauti na ule waliouzoea.

“Leo ilikuwa hali tofauti kwa sababu mazingira ya mchezo yalikuwa tofauti. Tunaendelea kuijenga timu na kila mazoezi yanatupa nafasi ya kuongeza mwelekeo mpya na suluhisho tofauti ndani ya timu,” amesema Pedro.

Kocha huyo amesema ingawa kulikuwa na mabadiliko kadhaa ya kimfumo, falsafa kuu ya timu hiyo iliendelea kubaki palepale.

Pedro amekiri kuwa walikutana na changamoto ya aina ya uwanja na mazingira ambayo hayakuwapa nafasi ya kucheza soka lao la kawaida la pasi na utulivu, hivyo walipaswa kucheza kwa nguvu zaidi na wakati mwingine kuwa wa moja kwa moja.

Kwa mujibu wa kocha huyo, hali ya hewa, ubora wa nyasi pamoja na ushindani wa wapinzani vilifanya mchezo huo kuwa mgumu, lakini bado ameridhishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake.

Ameongeza kuwa licha ya kutamani kuona umaliziaji bora zaidi katika baadhi ya nafasi walizotengeneza, bado anaamini timu yake ilionesha kiwango kizuri katika mazingira magumu.

Mbali na kuzungumzia mchezo, Pedro pia alitumia nafasi hiyo kuwapongeza mashabiki wa Yanga, maarufu kama Wananchi, kwa namna walivyoendelea kuisapoti timu yao bila kuchoka.

Related Articles

Back to top button