Ligi KuuNyumbani

Mtonyo wa Ulaya waipa kiwewe Coastal Union

DAR ES SALAAM: KISA ni mamilioni ya fedha kutoka moja ya klabu nje ya nchi, ndio imeleta utata mkubwa kati ya Klabu ya Simba na Coastal Union juu ya usajili wa beki Lameck Lawi ambaye tayari ametambulishwa kuwa ni mali ya Wekundu hao wa Msimbazi.

Jana Simba ilimtambulisha beki huyo wa kati kuwa mali yao kwa mkataba wa miaka mitatu kukiwa na kipengele cha kuongeza mkataba wa mwaka mmoja akitokea Coastal Union.

Baada ya utambulisho kumetokea sintofahamu juu ya viongozi wa timu hizo mbili, Simba ikidai kuwa imefuata taratibu kumsajili mchezaji huyo ambapo Coastal Union imeweka wazi kuwa kuna mambo hayajaenda sawa.

Kwa mujibu wa chanzo zilizofika mezani wa SpotiLeo ni kuwa kuna ofa nono kutoka barani Ulaya juu ya Lawi, hali ambayo inaleta utata na kuleta sintofahamu ndani ya klabu hizi mbili.

“Mazungumzo kati ya Simba na Coastal Union yalifanyika muda mrefu na walihitaji kiasi cha fedha Sh million 200 na kukaa meza moja kumalizana nao, yaliyoibuka sasa hivi ni suala la kuwepo kwa ofa kubwa kutoka moja ya timu barani Ulaya,” mtoa habari huyo amesema.

Amesema kilichokuwepo sasa ni suala la klabu hiyo kutoka Ulaya ambayo imeonyesha nia ya kumuhitaji mchezaji huyo hali ambayo Coastal Union wanahitaji kuona ofa hiyo inaenda kwao badala ya Simba waliomtambulisha mchezaji huyo.

Katika hatua nyingine Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Coastal Union, Omary Ayoub amesema kuwa hawana tena mpango wa kuendelea na mazungumzo na uongozi wa Simba juu ya kumuuza beki wao Lameck Lawi ambaye tayari ametambulishwa na Wekundu hao wa Msimbazi.

Ayoub amesema kulikuwa na mazungumzo na Simba kwa ajili ya makubaliano ya kumuuza mchezaji huyo lakini Simba hawajafuata makubaliano juu ya biashara ya nyota huyo.

“Ni kweli tulikuwa na mazungumzo na makubaliano yaliendelea vizuri lakini kuna  makusudio na makubaliano ambayo Simba hawajatekeleza, ukiachana na masuala ya fedha. Wameenda tofauti na utaratibu tuliokubaliana nao,” amesema katibu huyo.

Amesema Simba hawajafuata taratibu na wamesitisha mauzo ya mchezaji huyo na Lawi hataenda tena kucheza Simba na kuendelea kusalia kubaki ndani ya Coastal Union.

Naye Mjumbe wa Bodi ya Wakurugezi Simba, Cresentius Magori amesema Simba imefuata taratibu zote, haiwezi kwenda kinyume na makubalino ya Coastal Union, pamoja na sheria na kanuni za usajili zilizowekwa na mamlaka husika.

“Tulichelewa kumaliza pesa, tulilipa nusu lakini hadi June tulikuwa tumemaliza kulipa pesa yote ya usajili, tumemsajili Lawi kwa kufuata utaratibu, wangesema kama ukichelewa kulipa mkataba unavunjika, lakini hadi June tulikuwa tumemaliza kulipa pesa na nyaraka zote tunazo hata tukienda FIFA,” amesema Magori.

Amesema kilichotokea kuwepo na mvutano huu Coastal Union, Lawi amepata  ofa kutoka nje ya nchini hali iliyopelekea wakabadili maamuzi ya nyota huyo kutaka kumuuza na  kusahau makubaliano yaliyopo na Simba.

Related Articles

Back to top button