Kikapu

LeBron James afikia rekodi ya Parish

LOS ANGELES:NYOTA wa Los Angeles Lakers, LeBron James, ameifikia rekodi ya kihistoria ya Robert Parish ya kucheza mechi 1,611 katika Ligi ya NBA, rekodi ambayo ilikuwa imedumu kwa karibu miaka 30.

LeBron, mwenye umri wa miaka 41, alifikia idadi hiyo ya mechi Alhamisi usiku katika mchezo dhidi ya Miami Heat, akilingana na Parish ambaye alicheza kwa misimu 21 kuanzia mwaka 1976 hadi 1997.

Parish, ambaye sasa ana miaka 72, amesema LeBron anastahili kabisa kuivunja rekodi hiyo kutokana na namna anavyojitunza.

“Kama kuna mtu anayestahili kuvunja rekodi ya ‘iron man’, basi ni LeBron James. Anajitunza sana, anazingatia mazoezi, lishe na afya yake kwa kiwango kikubwa. Hilo linaonesha si tu uimara wangu wa zamani, bali pia uimara wake,” amesema Parish akizungumza na ESPN.

Mbali na kufikia rekodi hiyo ya mechi nyingi, LeBron tayari anashikilia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote wa NBA. Kufikia Jumatano, alikuwa na jumla ya pointi 43,210 katika maisha yake ya soka la kikapu.

Msimu huu, LeBron ameendelea kuonesha kiwango cha juu licha ya umri wake, akiwa na wastani wa pointi 21.4, asisti 6.8 na rebounds 5.6 kwa kila mchezo.

Katika maisha yake ya NBA, LeBron amewahi kuwa mchezaji wa All-Star mara 22, ametwaa ubingwa wa ligi mara nne na kushinda tuzo ya MVP mara nne.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button