
DR CONGO: Rais wa Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Congo FECOFOOT, Jean-Guy Blaise Mayolas, amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya ubadhirifu wa fedha za maendeleo ya soka.
Mahakama ya jinai mjini Brazzaville ilitoa hukumu hiyo baada ya uchunguzi wa miezi kadhaa kubaini kuwa Mayolas alihusika katika ubadhirifu wa zaidi ya dola milioni moja zilizotolewa na FIFA kwa ajili ya kuendeleza soka nchini humo.
Fedha hizo zilikuwa sehemu ya msaada uliotolewa wakati wa janga la COVID-19 na zililenga kusaidia programu za maendeleo ya soka, ikiwemo kuimarisha soka la wanawake pamoja na ujenzi wa miundombinu ya michezo. Hata hivyo, uchunguzi ulionyesha kuwa fedha hizo zilielekezwa katika matumizi binafsi kupitia miamala ya kifedha yenye utata na nyaraka bandia.
Mahakama pia ilimpata na hatia ya makosa mengine ikiwemo utakatishaji fedha, kughushi nyaraka na matumizi ya nyaraka bandia. Mayolas alihukumiwa akiwa hayupo mahakamani, huku mahali alipo kwa sasa ikiwa halijajulikana.
Katika kesi hiyo, maafisa wengine wawili wa juu wa shirikisho hilo Katibu Mkuu Badji Mombo Wantete na Mweka Hazina Raoul Kanda walihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kuhusika katika makosa hayo ya kifedha.
Uamuzi huo umetajwa kuwa moja ya hatua kali zaidi kuwahi kuchukuliwa dhidi ya kiongozi wa soka barani Afrika, na unatarajiwa kuibua mjadala mpana kuhusu uwazi na usimamizi wa fedha katika taasisi za michezo.




