Africa

Dau la Mzize kufuru

DAR ES SALAAM: OFISA Habari wa Yanga, Ali Kamwe ameweka wazi dau la mshambuliaji wao Clement Mzize anayewindwa na timu mbalimbali ndani na nje ya Bara la Afrika.

Star huyo anawindwa na timu hizo baada ya kuonesha uwezo mkubwa kwa misimu kadhaa ambapo Kamwe amesema Klabu inayomtaka iweke mezani Sh bilioni tano.

Kamwe amesema kiwango anachokionesha Mzize anazidi kujiongezea thamani kubwa katika dau lake ndio maana hawawezi kumuuza kwa bei ya chini kwani ni moja ya mastraika matata sana.

“Thamani ya Mzize sasa ipo juu wanachokipata wale wanaoenda kucheza Robo fainali kombe la Shirikisho Afrika (Simba), ndilo dau la nyota huyu,” amesema.

Kamwe amesema kila msimu thamani ya nyota huyo inazidi kuwa kubwa ndio maana haishangazi kuona timu mbalimbali zinatuma ofa zikiitaka huduma yake huku akiwaambia mashabiki wasiwe na wasiwasi wowote.

Licha ya Kamwe kutoweka wazi juu ya timu zilizofika mezani lakini taarifa zilizonaswa ni kuwa Al Attihad ya Libya, moja ya timu kubwa kutoka nchini Ubelgiji pamoja na Wydad Casablanca zinamtaka mchezaji huyo.

Kwa upande wake Kigogo mmoja ndani ya Yanga amesema kuwa, uwezekano mkubwa kwa straika huyo ni kwenda kukipiga Al Ittihad kwa sababu dau waliloliweka ni kubwa zaidi ya timu nyingine.

“Ukweli ni kwamba ofa zipo mezani na tayari uongozi upo katika harakati ya kukubali lakini uwezekano mkubwa ni kwenda kuichezea Al Ittihad kwani wameweka dau kubwa sana. Kuna ofa nyingine kutoka Ubelgiji lakini atakwenda Al Ittihad,” amesema.

Related Articles

Back to top button