Ni Man City na Real Madrid tena!

NYON:DROO ya hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imethibitisha pambano lingine kubwa kati ya Manchester City na Real Madrid katika hatua ya 16 bora. Huu ni mchuano ambao sasa umegeuka kuwa kama “fainali kabla ya fainali” kutokana na historia yao ya hivi karibuni.
Tangu mwaka 2020, timu hizi zimekutana mara kwa mara katika hatua za mtoano. Pambano lijalo litakuwa mara ya sita ndani ya miaka saba kukutana kwenye hatua kubwa za mashindano haya.
Kwa jumla, ndani ya mechi 15 za karibuni, Manchester City wameshinda mara tano, sare nne na kupoteza mara sita dhidi ya Real Madrid. Cha kuvutia zaidi ni kwamba magoli ni sawa kabisa 29 kwa 29, kitu kinachoonesha namna ambavyo wamekuwa wakilingana kwa kiwango.
Mwaka 2020 City waliitoa Madrid katika hatua ya 16 bora kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-2. Mwaka 2022 Madrid walirudisha mapigo kwenye nusu fainali kwa ushindi wa jumla ya 6-5 baada ya muda wa ziada, katika moja ya michezo ya kukumbukwa zaidi katika historia ya Champions League.
Mwaka 2023 City walilipiza kisasi kwa ushindi wa jumla ya 5-1 kwenye nusu fainali kabla ya kwenda kutwaa ubingwa. Mwaka 2024 na 2025 walikutana tena katika robo fainali na hatua ya play-off, mechi ambazo zilijaa mabao na drama ikiwemo mikwaju ya penalti.
Sasa wanakutana tena. Miaka saba, mechi zaidi ya kumi na mbili, idadi ya mabao sawa. Ni rahisi kusema kati yao, hakuna anayemmiliki mwingine hapa,atakayejichanganya ndio huyohuyo.
Nani atamtoa mwenzake mwaka huu?




