Pedro ampakulia ‘minyama’ Shekhan

DAR ES SALAAM : KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves, amemmwagia sifa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Shekhan Ibrahim kuwa ni miongoni mwa wachezaji wenye vipaji vikubwa ndani ya kikosi hicho.
Pamoja na sifa hizo, amemtaka Shekhan kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufikia kiwango cha juu zaidi.
Nyota huyo alikuwa ni miongoni mwa wachezaji walioifungia Yanga bao katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu jana.
“Ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa. Anatakiwa kujiamini zaidi, aendelee kufanya kazi kwa bidii na kuelewa tunachohitaji ndani ya timu,” amesema Pedro.
Kwa upande wake Shekhan amesema bao hilo limetokana na dua ambazo Mama yake amekuwa akimuombea na kuahidi kuwa iwapo ataendelea kupewa nafasi ya kucheza mashabiki watafurahia zaidi.
“Nikiendelea kupata nafasi wataniona huyu ndio Shekhan wa kweli,”amesema mchezaji huyo kijana kutoka Zanzibar.




