Africa

Gumbo: Morali Yanga juu, tunahitaji matokeo chanya

DAR ES SALAAM: UONGOZI wa Yanga SC umeeleza kuwa timu ipo katika hali nzuri kisaikolojia na kiufundi kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi dhidi ya FAR Rabat utakaochezwa nchini Morocco.

Akizungumza akiwa Morocco Mkuu wa Msafara wa Yanga na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Rogers Gumbo, alisema viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wamejipanga kikamilifu kwa ajili ya pambano hilo muhimu.

“Kama viongozi tumejipanga vizuri ili kufanikisha matokeo mazuri. Kwa aina ya benchi la ufundi na wachezaji tulionao tunaamini watafanya vizuri,” alisema Gumbo.

Aliongeza kuwa morali ndani ya kikosi ipo juu, hali inayotoa matumaini makubwa kwa Wananchi kuelekea mchezo huo wa ugenini.

“Wachezaji na viongozi wote wana morali kwa ajili ya mchezo. Tunawaomba Watanzania waendelee na dua ili tuweze kupata matokeo mazuri,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga ulieleza kuwa mchezaji mpya wa klabu hiyo, Buba Jammeh, aliyesajiliwa siku ya mwisho ya dirisha dogo la usajili, bado yuko nchini Gambia akishughulikia masuala ya hati yake ya kusafiria, na atajiunga na timu Dar es Salaam baada ya kukamilisha taratibu hizo.

Yanga inahitaji sare au ushindi katika mchezo dhidi ya FAR Rabat ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu hatua robo fainali.

 

Related Articles

Back to top button