Africa

CAF yaufungia Uwanja wa Mkapa

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeufungia kwa muda Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam kutokana na kupungua kwa ubora wa eneo la kuchezea (pitch).

Hatua hii inalenga kuhakikisha viwango vya viwanja vya mashindano ya kimataifa vinaendelea kuboreshwa kwa mujibu wa kanuni za CAF.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), CAF imetoa maelekezo kwa mamlaka husika kufanya maboresho ya haraka ili kuepusha uwezekano wa uwanja huo kufungiwa kwa muda mrefu zaidi.

Katika hatua nyingine, CAF imeitaka TFF kutuma jina la uwanja mbadala kwa ajili ya mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba  dhidi ya Al Masry, ambao ulikuwa umepangwa kufanyika katika dimba hilo mnamo Aprili 9. TFF imepewa hadi Machi 14 kuwasilisha jina la uwanja mbadala utakaotumika kwa mchezo huo.

Aidha, CAF imepanga kufanya ukaguzi wa uwanja huo mnamo Machi 20 ili kutathmini maboresho yatakayokuwa yamefanyika kabla ya kutoa maamuzi ya mwisho kuhusu matumizi yake kwenye mashindano ya kimataifa.

Hatua hii ya CAF inatoa changamoto kwa mamlaka za michezo nchini kuhakikisha viwanja vinatunzwa kwa viwango vinavyohitajika ili kuepusha athari kwa timu za Tanzania zinazoshiriki mashindano ya kimataifa.

Related Articles

Back to top button