Zimbwe Jr: Kocha Fadlu ni silaha yetu kubwa dhidi ya Stellenbosch

DAR ES SALAAM: NAHODHA na beki wa timu ya Simba, Mohammed Hussein maarufu kama Zimbwe Jr, amesema kuwa kocha wao Fadlu Davids ndiye silaha yao kubwa wanapoelekea kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini.
Simba inatarajiwa kuikaribisha Stellenbosch katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali utakaopigwa Aprili 20 katika Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, kabla ya mchezo wa marudiano utakaochezwa Aprili 27 nchini Afrika Kusini.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Zimbwe Jr amesema maandalizi yamefanyika kikamilifu, huku wakinufaika na maarifa ya kocha wao Fadlu ambaye anaifahamu vizuri soka ya Afrika Kusini.
“Fadlu ni silaha kubwa sana kwetu. Ametuelekeza mbinu za kukabiliana na wachezaji wao hatari, jinsi ya kucheza nyumbani na pia namna ya kujipanga ugenini. Anaijua falsafa ya soka la Afrika Kusini, jambo ambalo ni faida kwetu,” amesema Zimbwe Jr.
Beki huyo ameongeza kuwa malengo ya awali yalikuwa kufuzu hatua ya nusu fainali, na sasa dhamira kuu ni kutinga fainali kwa kuhakikisha wanashinda mechi ya nyumbani kwa idadi kubwa ya mabao bila kuruhusu kufungwa.
“Tumejipanga kuhakikisha tunamaliza kazi nyumbani. Tunahitaji ushindi Jumapili hii na kwenda Afrika Kusini kukamilisha kazi. Tunaamini tunaweza kufika fainali,” ameongeza nahodha huyo.