Nyumbani

Yanga: Tunataka rekodi ya nne

DAR ES SALAAM: YANGA imesema inalenga kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya nne mfululizo, huku ikiahidi kupambana kupata matokeo mazuri katika mchezo wa marudiano dhidi ya CFFA ya Madagascar utakaochezwa kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema timu hiyo haitaki kubweteka kwa ushindi wa mabao 4-0 ilioupata katika mchezo wa kwanza, badala yake inataka kukamilisha kazi kwa ushindi mwingine utakaothibitisha ubora wake.

“Bado haijaisha mpaka imalizike. Maandalizi yanaendelea vizuri na tunataka muendelezo wa rekodi bora. Tunakwenda kukamilisha kazi nyingine kwa kupambana ili tuweze kupata matokeo mazuri ya jumla na kuingia hatua ya makundi,” amesema Kamwe.

Amesema mchezo huo ni muhimu kwa Yanga na wachezaji wamehimizwa kupambana kwa nguvu zote, ikiwezekana kupata mabao mengi ili kufuzu kwa kishindo.

Kamwe amesema anaamini mashabiki wa Yanga watajitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu yao katika mchezo huo, akitumaini matokeo yatakayopatikana yataiwezesha klabu hiyo kuweka rekodi ya kufuzu hatua ya makundi mara nne mfululizo.

Hata hivyo, Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na changamoto ya majeraha kwa baadhi ya wachezaji wake, akiwemo kipa Djigui Diarra ambaye hatakuwepo kutokana na jeraha.

Kamwe amesema kutokuwepo kwa Diarra hakutoi sababu ya kuwa na wasiwasi, akieleza kuwa Abutwalib Mshery amekuwa akionesha kiwango kizuri na ana uwezo wa kulinda lango la timu hiyo, huku Hussein Masalanga akiwa chaguo jingine lenye uzoefu.

Wachezaji wengine wanaotarajiwa kukosekana kutokana na majeraha ni Duke Abuya, Yao Attohoula, Abdulnasir Casemiro na Saleh Hussein.

Habari njema kwa Yanga ni kurejea kwa beki wake Israel Mwenda katika utayari wa kucheza mechi za ushindani baada ya kupata ruhusa, ingawa uamuzi wa kumtumia utategemea benchi la ufundi.

Kamwe amesema wachezaji wengine wako imara na wanaendelea na maandalizi, wakilenga kuhitimisha mchezo huo kwa matokeo yatakayoiwezesha Yanga kufikia malengo yake katika michuano hiyo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button