Kwingineko

Maddison atoa gundu

Tottenham yavunja mwiko EPL

LONDON: TOTTENHAM Hotspur imevunja mwiko wa kutopata ushindi katika Ligi Kuu ya England (EPL) msimu huu baada ya kuichapa Coventry City mabao 3-1 Jumatatu usiku, katika mchezo ulioshuhudia kiungo mshambuliaji James Maddison akirejea kwa kishindo kwenye kikosi cha kwanza.

Maddison, aliyeanza kwa mara ya kwanza baada ya miezi 17, aliifungia Tottenham bao la kwanza dakika ya 14 kwa shuti la kuvutia lililomshinda kipa Carl Rushworth. Bao hilo lilitokana na pasi ya Mohammed Kudus, aliyemwandalia nafasi nzuri kiungo huyo.

Hata hivyo, Coventry ilisawazisha dakika ya 49 kupitia Jack Rudoni, aliyenufaika na mpira uliomrudia baada ya shuti lake la kwanza kuzuiwa. Tottenham ilijibu dakika ya 58 kupitia Omar Marmoush, aliyepiga shuti kali na kuirejesha timu yake mbele.

Katika dakika za nyongeza, Ben Davies alifunga bao la tatu na kuhakikisha Tottenham inaondoka na pointi zote tatu. Ushindi huo umempa nafuu kocha Roberto De Zerbi, aliyekuwa akikabiliwa na presha kutokana na mwenendo mbaya wa timu yake mwanzoni mwa msimu.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Maddison mwenye umri wa miaka 29 alisema alitaka kuonesha uwezo wake na mchango anaoweza kuutoa kwa timu baada ya kukaa muda mrefu nje ya kikosi cha kwanza. Alieleza kuwa bado ana miaka mingi ya kucheza soka na anaamini anaweza kusaidia Tottenham kuboresha matokeo yake.

Maddison alikuwa nje kwa muda mrefu baada ya kupata jeraha la kupasuka kwa kano ya mbele ya goti la kulia (ACL) Agosti 2025. Katika mchezo huo, Dejan Kulusevski pia alirejea kwenye kikosi cha siku ya mechi baada ya kukosa muda mwingi kutokana na majeraha.

Kabla ya ushindi huo, Tottenham ilikuwa mkiani mwa msimamo wa EPL na haikuwa imepata ushindi wa ligi msimu huu. Ushindi dhidi ya Coventry umeipandisha hadi nafasi ya 16 na kumpa De Zerbi nafasi ya kuijenga upya timu hiyo, huku akitarajia kuendeleza matokeo mazuri katika michezo ijayo ili kuepuka hatari ya kushuka daraja.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button