Makocha Perez, Iraola kukutana UEFA

LIVERPOOL: KOCHA wa Liverpool, Andoni Iraola, amesema mchezo dhidi ya Villarreal inayofundishwa na rafiki yake wa muda mrefu, Inigo Perez, utakuwa wa kipekee watakapokutana katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye Uwanja wa Anfield Jumanne.
Makocha hao wawili raia wa Hispania wamefahamiana tangu walipokuwa wachezaji vijana katika akademia ya Athletic Bilbao, kabla ya kucheza pamoja katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo.
Baada ya Perez kustaafu soka, Iraola alimchukua kuwa msaidizi wake alipokuwa akiinoa Rayo Vallecano ya Madrid, ambako walifanya kazi pamoja na kupitia changamoto mbalimbali.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Iraola alisema ana furaha na fahari kukutana na rafiki yake katika mashindano makubwa ya Ulaya, akieleza kuwa wamejenga uhusiano wa karibu kwa miaka mingi.
Alisema kwa kawaida huzungumza na Perez kuhusu soka, maisha na familia, lakini mawasiliano yao yamepungua kadiri mchezo unavyokaribia ili kila mmoja ajikite katika maandalizi ya timu yake.
Iraola, mwenye umri wa miaka 44, alifichua kuwa alipokuwa Bournemouth alijaribu kumleta Perez England ili awe msaidizi wake, lakini mpango huo ulishindikana baada ya rafiki yake kunyimwa kibali cha kufanya kazi nchini humo.
Pamoja na kushindwa kufanya kazi pamoja England, Iraola alisema anafurahi kuona Perez akipata nafasi ya kuinoa Villarreal na kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mchezo huo unawakutanisha marafiki wa muda mrefu ambao sasa watakuwa wapinzani kwa dakika 90, kila mmoja akilenga kuiongoza timu yake kupata ushindi katika michuano hiyo.




