AFD, NBA Africa wanoa walimu 100 kikapu

NAIROBI: WALIMU 100 wa somo la elimu ya viungo nchini Kenya wamepatiwa mafunzo ya ufundishaji wa mpira wa kikapu unaojumuisha watoto wenye ulemavu, kwa lengo la kuhakikisha wanapata fursa sawa ya kushiriki katika michezo.
Mafunzo hayo ya siku moja yalifanyika Jana katika uwanja wa mpira wa kikapu wa Fam Sports Arena, Kitengela, yakiandaliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa kushirikiana na NBA Africa kupitia mpango wa Basketball Experience.
Programu hiyo, inayojulikana kama Basketball Experience Disability Inclusion (BE-DI) Teachers Awareness Day, ililenga kuwajengea walimu uwezo wa kufundisha misingi ya mpira wa kikapu huku wakizingatia mahitaji ya watoto wenye uwezo na changamoto mbalimbali za kujifunza.
Mafunzo hayo yalihusisha vipindi vya darasani na mazoezi ya uwanjani kwa kutumia mtaala wa Jr. NBA, yakisisitiza mbinu salama, zinazolingana na umri wa watoto na zinazozingatia ujumuishi.
Kupitia mbinu za ufundishaji zinazoweza kurekebishwa kulingana na mahitaji ya watoto, shughuli zinazofikika kwa wote na usanifu wa mtaala jumuishi, mpango huo unalenga kuondoa vikwazo vinavyowazuia watoto wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika michezo.
Aidha, programu hiyo ilijumuisha mafunzo ya stadi za maisha yaliyotolewa kwa ushirikiano na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya. Mafunzo hayo yalisisitiza nafasi ya michezo katika kukuza ushirikiano, ustahimilivu, uongozi, uelewa wa masuala ya afya na uwajibikaji wa kijamii.
AFD na NBA Africa zimesema mpango mpana wa Basketball Experience unatumia mpira wa kikapu kuendeleza elimu, stadi za maisha na fursa jumuishi kwa vijana katika jamii mbalimbali.
Kupitia kuwajengea walimu uwezo wa kufundisha watoto wenye mahitaji na uwezo tofauti, mpango huo unalenga kujenga mazingira ya michezo ambayo watoto wanaweza kujifunza, kucheza na kukua pamoja, ndani na nje ya uwanja.
Hatua hiyo inaweka msisitizo katika kuhakikisha watoto wenye ulemavu hawabaguliwi au kunyimwa nafasi ya kushiriki michezo, huku walimu wakipewa mbinu za kuandaa shughuli zinazowezesha kila mtoto kushiriki kulingana na uwezo na mahitaji yake.




