Yanga SC yatokwa udenda kwa Khomein Aboubakari
DAR ES SALAAM: KIPA namba moja wa Singida Black Stars, Khomein Aboubakari anatajwa kutua katika kikosi cha Yanga kwenda kuongeza nguvu kuchukuwa nafasi ya Metacha Mnata.
Taarifa zilizoifikia Spotileo zinasema uongozi wa Yanga unaongozwa na rais Hersi Said wako katika mchakato wa kuhitaji huduma ya kipa huyo alionyesha ubora mzuri kwenda kuchukuwa nafasi Metacha amepewa ‘THANK YOU’.
“Yanga inahitaji kipa mwingine anayekuja kuchukuwa nafasi ya Metacha, baada ya kushindwa kumpata huduma ya Yona Amosi kipa wa Tanzania Prison, Khomein amepita katika mchakato huyo na kinachosubiriwa muda tu,” amesema mtoa habari huyo.
Alipotafutwa Ofisa habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza amesema hapo awali walikuwa na mpango huo baada ya Yanga na timu nyingine kuhitaji huduma ya kipa huyo.
Amesema kwa sasa hawezi kusema neno lolote hadi hapo watakapomaliza usajili na kufanikisha wachezaji ambao wanafanya nao mazungumzo kulingana mapendekezo ya benchi la ufundi.
“Kama tutafanikiwa kupata kipa nje ya nchi, tukikosa basi Khomein ataendelea kusalia ndani ya kikosi ukizingatia msimu ulioishia alionyesha kiwango kizuri na alikuwa tegemeo kwetu,” amesema Ofisa huyo ambaye hakuweka wazi jina la kipa wa kigeni wanayemuwinga.