Yanga, JKT wanaingia vita ya uongozi

DAR ES SALAAM: YANGA na JKT Tanzania wanaingia kwenye vita ya uongozi watakapokutana kesho katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC .
JKT ndiye kinara kwa pointi 28 katika michezo 16 tofauti ya pointi tatu dhidi ya Yanga ambaye pia, yuko nyuma michezo saba.
Huenda wanajeshi wakashushwa kama wataruhusu kufungwa maana yake watalingana pointi sawa kitakachowatofautisha ni mabao yakufungwa na kufunga JKT imefunga mabao 18 na kufungwa 10 huku Yanga imefunga mabao 22 na kufungwa mawili.
Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, amesema mchezo huo utakuwa mgumu, lakini malengo makubwa ya timu hiyo ni kuhakikisha inaondoka na pointi tatu.
Kamwe amesema wanatambua ubora wa wapinzani wao ambao wana wachezaji wenye uzoefu na kiwango kizuri, hivyo watalazimika kucheza kwa tahadhari kubwa katika kuhakikisha wanapata matokeo wanayoyahitaji.

“Ni mechi ngumu, JKT wana wachezaji wazuri na wenye uzoefu. Kikubwa kwetu ni kuchukua tahadhari zote lakini lengo letu ni pointi tatu,” alisema Kamwe.
Kwa upande wa JKT Tanzania, Msemaji wa klabu hiyo Masau Bwire amesema wanatambua ukubwa wa mchezo huo na ubora wa Yanga, lakini wamefanya maandalizi maalum kuhakikisha wanabaki kileleni.
Aliongeza kuwa presha ya kuwania nafasi ya juu haibadilishi malengo yao ya kutafuta ushindi katika kila mchezo.




