Kuogelea

Jangwani, Muntazir zang’ara kuogelea wenye ulemavu

DAR ES SALAAM: TIMU za kuogelea kutoka Shule za Sekondari Jangwani na Shule maalum ya Al Muntazir zote za Dar es Salaam zimeng’ara kwenye mashindano ya pili ya taifa ya kuogelea kwa watu wenye ulemavu baada ya wachezaji wao kufanya vizuri.

Katika mashindano hayo yaliyofanyika kwenye Bwawa la kuogelea la Shabaan Robert, Upanga Dar es Salaam leo chini ya Chama cha Kuogelea kwa watu wenye ulemavu (TPSA), kwa upande wa wanawake Jangwani iliyokuwa na wachezaji zaidi ya 20 imepata jumla ya pointi 392 ikifuatiwa na Pigec 60 na tatu ni Al Muntazir yenye pointi 40.

Kwa upande wa wanaume timu inayoongoza ni Shule ya Sekondari Pugu iliyopata pointi 244, ikifuatiwa na Al Muntazir 123, St Joseph 85, Pigec 49 na Stigrays 40.

Mchezaji Luciano Masika kutoka klabu ya Stingray mwenye ulemavu wa mguu mmoja amesema ushindani ni mzuri japo sio sana kwani alitamani kushindana na mwenye uwezo kama wake ili kwenda sambamba.

“Tanzania hakuna anayeweza kunishinda, natamani kupata mshindani mzuri kwasababu waliopo nimewashinda wote na kufanya vizuri, naomba serikali iendelee kuwekeza kwenye mchezo huu na wadau wengine waongeze nguvu kuwasaidia kutimiza ndoto zao,”amesema.

Rais wa Kamati ya Paralimpiki Tanzania (TPC) Tuma Dandi amewapongeza watoto wenye ulemavu kwa ushiriki wao kwenye mashindano akisema wanatamani jamii iwape faraja.

Amesema kutokana na maumbile yao sio kwamba hawawezi kufanya kitu kabisa wanafanya vizuri.
“Nimpongeze Katibu Mkuu wa TPSA Ramadhan Namkoveka kwa kutumia muda wake mwingi kujitoa kiasi cha familia yake kumkosa kwa ajili ya michezo, yeye sio mlemavu ila anapenda kutoa faraja,”amesema.

Mwakilishi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Nicholas Mihayo amewapongeza waandaaji wa mashindano hayo akisema kilichofanyika kinapaswa kuigwa na vyama vingine vya michezo.

“Michezo ipo mingi lakini ni mara chache ukakuta vijana wenye mahitaji maalum kama tunachokiona hapa, kwa hiyo ikiwezekana vyama vingine vya michezo ikifanya kama hivi itakuwa ni vizuri sana, kwani wapo wengi nyumbani na shuleni na wengi wanapenda kushiriki katika michezo,”amesema.
Amewaasa wazazi wenye watoto wenye ulemavu wawatoe wawape nafasi kama hiyo, serikali na vyama vya michezo wapo kwa ajili ya kuwasaidia.
Mwisho

Related Articles

Back to top button