Waogeleaji 70 wenye ulemavu kushindana Dar
DAR ES SALAAM:WAOGELEAJI 70 wenye ulemavu wanatarajiwa kushindana Jumamosi ya wiki hii katika mashindano ya pili ya kitaifa ya kuibua vipaji yatakayofanyika katika bwawa la kuogelea la Shabaan Robert, Upanga Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Chama cha Kuogelea kwa watu wenye ulemavu (TPSA) Ramadhan Namkoveka ameiambia SpotiLeo kuwa waogeleaji wenye changamoto mbalimbali ikiwemo ulemavu wa viungo, ngozi, macho na usonji wataonesha vipaji vyao.
“Kamati yetu ya maandalizi ya mashindano ikiongozwa na Thauriya Diria akisaidiwa na Clara Kiziga inafanya kila juhudi kuhakikisha mashindano haya yanafanyika kwa mafanikio makubwa,”amesema.
Amesema wachezaji watakaofanya vizuri watachagauliwa kwenye timu ya Taifa kwa ajili ya kupatiwa mafunzo zaidi na kuweza kushiriki mashindano kadhaa ya kimataifa.
Namkoveka amesema changamoto ni nyingi na bila ya msaada wa wadau mbalimbali wakiwemo familia ya kuogelea, makampuni na watu binafsi hawataweza kufanikiwa na kufikia malengo waliyojiwekea.
“Tunawashukuru wanaotusaidia na kutudhamini wakiwemo Tiba Hospital, Tanzania Paralympic Committee (TPC), Tanzania Swimming Association, Tanzania Beach Life Guards, Champion Rise, Iprint, Pepsi, Taliss Swimming Club, Lions Club of Dar es Salaam, Jou Ultra Sports, World Arya Vysya Mahasabha, Tanzania Vibhag, The Flames, Saifee Hospital na Blue Dot Insurance Agency,”ameongeza.
Mgeni Rasmi wa mashindano hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Kamati ya Paralimpiki Tanzania (TPC) Provian Dandi.
Watatumia mashindano hayo kupima afya kwa wananchi wote ambao watapenda kujua afya zao bure.