Kwingineko

Kombe la Dunia kusafirishwa kifahari

NEW YORK: Kombe la Dunia la FIFA litawasili katika Uwanja wa New York-New Jersey kwa staili ya kipekee baada ya kuwekwa ndani ya sanduku maalum lililobuniwa na kampuni maarufu ya mitindo ya kifahari ya Ufaransa, Louis Vuitton, ambayo kwa mara nyingine imepewa jukumu la kutengeneza kifaa cha kubebea tuzo hiyo yenye thamani kubwa zaidi katika soka duniani.

Sanduku hilo limepambwa kwa alama ya herufi ‘V’ ya dhahabu, inayowakilisha neno ‘Victory’ (Ushindi) pamoja na jina la ‘Vuitton’, huku likiwa na nembo maarufu ya kampuni hiyo na kingo zilizofunikwa kwa shaba yenye rangi ya dhahabu. Ndani yake kumewekwa ngozi ya rangi ya beige pamoja na nembo maalum inayoashiria ushirikiano kati ya Louis Vuitton na FIFA.

Hii ni mara ya tano mfululizo kwa Louis Vuitton kutengeneza sanduku rasmi la kubebea Kombe la Dunia, baada ya kufanya hivyo katika michuano ya mwaka 2010, 2014, 2018, 2022 na sasa 2026. Ushirikiano huo umeifanya kampuni hiyo kuwa sehemu ya historia ya moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo duniani.

Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Louis Vuitton, Pietro Beccari, amesema kwa zaidi ya muongo mmoja kampuni hiyo na FIFA zimekuwa zikishirikiana kwa lengo la kuenzi ubora na kuonesha jinsi michezo inavyoweza kuunganisha watu duniani. Amesema ni heshima kubwa kwa kampuni hiyo kuendelea kuaminiwa kubeba ishara muhimu zaidi ya mafanikio katika soka.

Mbali na Kombe la Dunia, Louis Vuitton pia hutengeneza masanduku maalum ya kubebea mataji ya mashindano makubwa ya Formula One, huku kampuni ya Tiffany & Co. ikiwa ndiyo inayotengeneza kombe la Vince Lombardi linalotolewa kwa mabingwa wa Super Bowl nchini Marekani.

Kombe la Dunia, ambalo kwa kawaida huhifadhiwa katika Makumbusho ya FIFA jijini Zurich, Uswisi, litasafirishwa kwa hadhi hiyo maalum kuelekea fainali ya Kombe la Dunia 2026, likiendelea kuwa moja ya alama zinazovutia zaidi katika mchezo wa soka duniani.

Related Articles

Back to top button