Mashabiki wa Salman Khan washtushwa na muonekano wake wa sasa

MUMBAI, INDIA: Muonekano wa hivi karibuni wa staa mkubwa wa filamu za Bollywood, Salman Khan, umeibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya mashabiki wake kuonesha wasiwasi kuhusu afya yake kutokana na mabadiliko yaliyoonekana kwenye mwili wake.
Video na picha za muigizaji huyo zilisambaa kwa kasi mtandaoni baada ya kuonekana katika shughuli ya kijamii mjini Mumbai, huku jambo lililowavuta wengi likiwa ni muonekano wake wa kupungua uzito ukilinganishwa na alivyozoeleka kuonekana katika miaka iliyopita.
Salman Khan alihudhuria hafla ya kutembelea ofisi za Slum Rehabilitation Authority (SRA) mjini Mumbai, ambapo alishiriki katika uzinduzi wa kituo cha kisasa cha ukusanyaji na uhakiki wa taarifa pamoja na kukabidhi funguo za nyumba kwa baadhi ya wanufaika wa mpango huo.
Hata hivyo, badala ya tukio hilo kuzungumziwa zaidi, macho ya mashabiki yalielekezwa kwenye muonekano wa mwigizaji huyo mwenye umri wa miaka 60, huku baadhi yao wakisema waliona kama amepungua mwili na kuonekana tofauti na kawaida.
Kupitia mitandao ya kijamii, mashabiki wengi walitoa ujumbe wa kumtakia afya njema na kuuliza kama kuna jambo lolote linaloendelea kuhusu hali yake ya kiafya. Baadhi waliandika kuwa walishangazwa na mabadiliko hayo na kutamani kujua kama staa huyo yuko salama.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna taarifa rasmi kutoka kwa Salman Khan, familia yake au timu yake ya usimamizi inayothibitisha kuwa ana tatizo lolote la kiafya. Watu wengi wameendelea kusisitiza kuwa mabadiliko ya mwonekano pekee hayawezi kuthibitisha uwepo wa ugonjwa.
Salman Khan ni mmoja wa waigizaji wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini India, akiwa na miongo kadhaa ya mafanikio katika tasnia ya Bollywood kupitia filamu zilizovunja rekodi kama ‘Bajrangi Bhaijaan’, ‘Sultan’ na ‘Tiger’.
Muonekano wake mpya umeendelea kuwa gumzo kwa sababu kwa muda mrefu amekuwa akijulikana kwa umbo lake la misuli na sura yake iliyokuwa sehemu ya utambulisho wake kama mmoja wa mastaa wakubwa wa filamu za India.
Kwa sasa, mashabiki wake wanaendelea kusubiri taarifa zaidi huku wengi wakimtumia ujumbe wa kumuunga mkono na kumtakia afya njema, wakisema wanathamini mchango wake mkubwa katika burudani ya India na dunia.




