Rapa Alley Boy afariki dunia

ATLANTA: Dunia ya muziki wa hip hop imegubikwa na huzuni baada ya taarifa za kifo cha rapa maarufu wa Atlanta, Alley Boy, ambaye jina lake halisi ni Curt Freeman, kuanza kusambaa kupitia watu mbalimbali ndani ya tasnia hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa zinazotolewa na baadhi ya watu wa karibu na eneo la muziki wa hip hop nchini Marekani, Alley Boy ameripotiwa kufariki huku madai yakieleza kuwa chanzo cha kifo chake ni ugonjwa wa figo kushindwa kufanya kazi (kidney failure).
Hata hivyo, hadi sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na familia yake au wawakilishi wake kuthibitisha sababu halisi ya kifo hicho.
Taarifa za kifo cha rapa huyo zilisambaa baada ya baadhi ya watu maarufu katika tasnia ya hip hop kutoa salamu za rambirambi kupitia mitandao ya kijamii. Miongoni mwa waliotajwa kuthibitisha taarifa hizo ni baadhi ya watu waliokuwa karibu naye katika muziki wa Atlanta, akiwemo DJ Scream, Big Bank, Roco na Ralo.
Mashabiki wa Alley Boy wamepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa, huku mamia yao wakituma ujumbe wa maombolezo kwenye mitandao ya kijamii. Wengi wamemkumbuka kama msanii aliyekuwa na mchango mkubwa katika kukuza muziki wa trap kutoka Atlanta Marekani.
Alley Boy alikuwa mmoja wa majina yaliyohusishwa sana na harakati za muziki wa trap mjini Atlanta tangu mwishoni mwa miaka ya 2000. Alijulikana zaidi kupitia lebo ya muziki ya Duct Tape Entertainment, ambayo ilipata umaarufu mkubwa katika eneo la Southern Hip Hop.
Katika safari yake ya muziki, alifanya kazi na baadhi ya majina makubwa katika hip hop kama Meek Mill, Future, Yo Gotti, Young Jeezy na Gucci Mane, jambo lililoongeza heshima yake ndani ya tasnia, mchango wa Alley Boy katika muziki wa Atlanta tayari umeanza kuenziwa na mashabiki na wasanii wenzake wanaomkumbuka kama mmoja wa watu waliosaidia kujenga msingi wa muziki wa trap katika miaka ya hivi karibuni.
Endapo taarifa hizo zitathibitishwa, kifo cha Na F, maarufu kama Alley Boy, kitakuwa pigo jingine kwa jamii ya hip hop ambayo imepoteza mastaa kadhaa waliokuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza utamaduni wa muziki huo.




