Hispania yatwaa kombe la dunia 2026 kwa kishindo

MAREKANI: Hispania imeandika ukurasa mpya katika historia ya soka duniani baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia 2026 kwa kuichapa Argentina bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa MetLife, New Jersey.
Ushindi huo umeipa Hispania taji lake la pili la dunia, miaka 16 tangu ilipotwaa ubingwa wake wa kwanza mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
Mchezo huo uliokuwa wa kasi na ushindani mkubwa uliwashuhudia Wahispania wakitawala sehemu kubwa ya mchezo, huku Argentina ikijikuta ikipata wakati mgumu kupenya safu ya ulinzi iliyokuwa imara ambapo dakika 00 za mchezo ziliisha bila kufungana.
Mshambuliaji Ferran Torres ndiye aliyeleta tofauti ya mechi hiyo na kuiibuka shujaa wa Hispania baada ya kufunga bao la ushindi katika dakika za nyongeza na kuzamisha ndoto za Argentina kutetea ubingwa wake wa dunia.
Ushindi huo unaifanya Hispania kurejea kileleni mwa soka la dunia kwa mara ya kwanza tangu mafanikio yake ya mwaka 2010. Aidha, umeonesha ubora wa kizazi kipya cha wachezaji wa taifa hilo kilichoongozwa na nyota Lamine Yamal, Rodri na Nico Williams, ambao walitoa mchango mkubwa katika safari ya kuelekea ubingwa huo.
Kwa Argentina, ilikuwa ni siku ya majonzi kwa nahodha Lionel Messi, ambaye wengi wanaamini huu unaweza kuwa mchezo wake wa mwisho wa Kombe la Dunia. Licha ya uzoefu wake mkubwa, Argentina ilishindwa kuvunja ukuta wa safu ya ulinzi ya Hispania.
Mbali na kutwaa kombe, Hispania imeweka rekodi nyingine ya kipekee baada ya kumaliza mashindano ikiwa imeruhusu bao moja pekee katika mechi zote nane za Kombe la Dunia 2026.
Mafanikio hayo yameifanya timu hiyo kutajwa kuwa moja ya mabingwa waliokuwa na safu bora zaidi ya ulinzi katika historia ya mashindano hayo.
Fainali hiyo iliyoshuhudiwa na zaidi ya mashabiki 80,000 katika Uwanja wa MetLife imehitimisha rasmi Kombe la Dunia la kwanza kushirikisha timu 48. Mashindano hayo yameacha kumbukumbu nyingi za kihistoria, lakini ushindi wa Hispania utaendelea kukumbukwa kama mwanzo wa enzi mpya ya ubabe wa soka la kimataifa na kurejesha hadhi ya “La Roja” kwenye kilele cha mchezo huo duniani.




