Mzee Mpili kuzikwa leo saa 10

PWANI: ALIYEKUWA mwanachama maarufu wa Klabu ya Yanga, Haji Omari Ramadhani Mpili, anatarajiwa kuzikwa leo Jumatatu Wilaya Ikwiriri, Pwani.
Uongozi wa Yanga umetangaza taarifa hiyo baada ya kifo chake kilichojiri usiku wa jana Septemba 27, wakati akipatiwa matibabu kwenye kituo cha afya huko Ikwiriri.
Imeelezwa Mzee Mpili alikuwa akisumbuliwa na maradhi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mgongo, kiuno na magonjwa ya uzee.
Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika saa 10:00 jioni katika Makaburi ya Msikiti Mkuu, Wilaya ya Ikwiriri, Mkoa wa Pwani.
Uongozi wa Yanga umetoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wadau wa mpira kwa msiba huo, huku ukiwaomba kuwa na subira na utulivu katika kipindi hiki kigumu.
Mzee Mpili alijizolea umaarufu miaka ya hivi karibuni kutokana na kauli zake tata za utani kwa wapinzani na mikwara yenye kufurahisha na kudumisha utani wa soka nchini.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.




