Muziki

Tuzo za muziki wa injili zazinduliwa

DAR ES SALAAM: TUZO za Tanzania za muziki wa Injili  (TGMA) 2025 zimezinduliwa rasmi leo, zikiwa na vipengele zaidi ya 20 ambavyo vitashindaniwa na waimbaji wa nyimbo za Injili nchini.

Uzinduzi huo umefanyika katika Ukumbi wa Serena Hotel,  ambapo Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa nchini BASATA, Dk. Kedmon Mapana, amepongeza hatua hiyo nzuri iliyofikiwa na kusema kuwa tuzo hizo zitaleta hamasa kwa wasanii wa Injili kufanyakazi kwa bidii.

“TGMA 2025 inatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kutambua na kuthamini mchango wa wasanii wa Injili, huku ikitoa fursa kwa vipaji vipya kung’ara katika tasnia hiyo.

“TGMA 2025 ni jukwaa muhimu kwa wasanii wa Injili kuonesha vipaji vyao na kuhamasisha jamii kupitia muziki wa kiroho. Tunahimiza wasanii kuzingatia maadili, ubunifu, na ubora katika kazi zao,” amesema Dk Mapana.

Miongoni mwa matukio muhimu katika uzinduzi huo ni kutangazwa kwa vipengele vya tuzo hizo, ambavyo ni pamoja na Wimbo Bora wa Kuabudu wa Mwaka, Msanii Bora wa Muziki wa Injili wa Mwaka, Albamu Bora ya Injili, na Tuzo Maalum ya Gospel Music Lifetime Achievement Award.

Pia, imeelezwa kuwa wasanii wote wanaotaka kushiriki katika tuzo hizi wanapaswa kuwa wamesajiliwa rasmi na BASATA ili kuhakikisha uwajibikaji na ufanisi katika tasnia ya muziki wa Injili nchini.

Hafla hiyo imehudhuriwa na wasanii wa muziki wa Injili, wadau wa tasnia ya muziki, waandishi wa habari, pamoja na viongozi wa serikali.

Related Articles

Back to top button