BurudaniMuziki

Lady Jaydee akumbusha wasanii kurudi njia kuu

SASA imekuwa kawaida kwa wasanii wa Bongo Fleva kuimba Amapiano.

Midundo ya kwenye nyumba zao, aina ya uchezaji wa kugeuza macho na kupandisha mabega juu huku wakichezesha mikono kuipeleka juu na chini ndio imekuwa aina pendwa ya uchezaji kwa wasanii wa Bongo Fleva.

Hata wale ambao haikufikiriwa kuimba Amapiano nao wameingia kwenye mtego huo na sasa wote wanaimba lugha moja, ni Amapiano mwanzo mwisho.

Amapiano asili yake ni Afrika Kusini na Amapiano hasa ni neno la Kizulu au Kixhosa ambayo tafsiri yake ni piano. Hiyo ni aina ya muziki iliyojitokeza Afrika Kusini mwanzoni mwa mwaka 2010.

Ukisikiliza vizuri muziki huo unagundua ni mchanganyiko wa aina kadhaa za muziki ukiwemo House na Jazz. Amapiano ilianzishwa na mchango wa vikundi vya wasanii na watayarishaji wa muziki nchini Afrika Kusini.

Kwa hakika Afrika Kusini imefanikiwa kuteka soko la muziki na sasa Tanzania, hakuna tena mchiriku wala singeli kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, mchiriku umesahaulika kila mtu anakwenda na fashion ya Amapiano.

Kama ilivyochangamka amapiano kwa sasa, ndivyo hata singeli na mchiriku ilikuwa hivyo.
Mchiriku, singeli ulikuwa muziki wenye vionjo vya asili ya Tanzania na popote ulipopigwa haikuwa na shida kujua huo ni muziki kutoka wapi.

Sasa hivi amapiano ni muziki wa Afrika Kusini lakini wasanii kutoka Tanzania ndio wameuchangamkia pengine kuliko wasanii wote wa Afrika Mashariki na Kati. Wanachofanya wasanii ni kama usaliti kwa mchiriku na singeli havikuwahi kufanya vibaya bado vikiwa kwenye uhai wake wasanii wameviacha na kurukia amapiano.

Wimbo kama Hujanikomoa kutoka kwa Harmonize, na nyimbo kadhaa za Mzee wa Bwax, Dulla Makabila, Sholo Mwamba na Meja Kunta ni aina ya nyimbo ambazo kuzisikia kwa sasa itakuwa ngumu kutokana na soko kutekwa na amapiano na mashabiki kulewa kwenye muziki huo.

Hata sijui kwanini wasanii wetu waliamua kubadilika na kusaliti mchiriku na singeli, miziki yenye aina ya midundo yenye mzuka pia inayomfanya shabiki kucheza kwa namna yake, wasanii wamechagua kutikisa vichwa, mabega na kugeuza macho juu chini.

Baada ya kusikia ‘vurugu’ za amapiano kwa takribani miaka mitatu sasa kutoka kwa wasanii mbalimbali wa kike na wa kiume, dada mkubwa kwenye Bongo Fleva, Judith
Wambura ‘Lady Jaydee’ amekuja na kitu tofauti kuwakumbusha wadogo zake kwamba
wabaki njia kuu.

Katikati ya wiki hii Jaydee maarufu kama Komando ametoa wimbo wake unaoitwa mambo matano. Kwenye wimbo huu Jide amezungumzia mapenzi akimpa taarifa mwanaume
aliyemzingua kwamba yeye maisha yake yanasonga na wala hana presha yoyote huku yule mwanaume akiwa kwenye hali ngumu.

Achana na ujumbe ulio kwenye wimbo, hapa nazungumzia namna Jide alivyobaki kuwa yule yule hata wakati huu wa mlipuko wa amapiano ambapo hadi baadhi ya wasanii wenzake wakongwe pia wameshindwa kuvumilia na kuingia kwenye mtego.

Sauti na mapigo ya wimbo huo vimetulia na havichoshi masikioni mwa msikilizaji na shabiki wa muziki. Nimeona hata mapokeo ya wimbo yamekuwa makubwa wengi wakipongeza kwamba sasa watapumzika kusikiliza amapiano baada ya kusikiliza kwa takribani miaka miwili mfululizo.

Lakini kabla ya mambo matano, Jide pia takribani wiki tatu zilizopita alitoa wimbo wa taratibu unaokwenda kwa jina la Ndoto Yangu aliomshirikisha Rama Dee. Wimbo wa taratibu unaosikilizika amebaki kwenye njia ileile ambayo hakuna shaka kwamba hajutii na wala hatamani kuibadilisha.

Ujio wa Jide umedhihirisha uzoefu na ukongwe wake kwenye soko la muziki wa kizazi kipya
kwani pamoja na ‘uvamizi’ wa amapiano hakuogopa badala yake amekuja kama alivyozoeleka tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Heshima kwa Jide imeanza miaka mingi tangu alipoanza kutamba na albamu yake ya kwanza ya Machozi iliyobamba vilivyo miaka hiyo. Historia haifutiki kwani albamu hiyo ilimfanya Jide kuwa msanii wa kwanza mwanamke kutengeneza albamu kwa fedha nyingi.

Miaka ya karibuni alivuma na nyimbo kadhaa ukiwemo Ndindindi ambao nao pia ulifanya vizuri kama ilivyo kawaida kwenye nyimbo zake. Jide anadhihirisha hatetereki kwani miaka yote amekuwa hivyo licha ya kukusanya tuzo nyingi kwa wasanii wa kike nchini.

Aliwahi kuchukua tuzo ya Msanii Bora wa Kike wa Tanzania kwa muziki wa R&B mwaka 2002, ambapo pia alitumbuiza katika tamasha kubwa kwa wakati ule la Kora. Mwaka 2005 alipata tuzo ya video bora ya msanii wa kike kwa Afrika Kusini.

Baadhi ya albamu za msanii huyo ni Machozi, Binti, Moto, Shukrani, Ya 5. The Best of Lady Jaydee, Nothing But The Truth na Woman. Wasanii wa kike na wa kiume bado kuna mengi ya kujifunza kwa wasanii wakongwe kama Lady Jaydee.

Related Articles

Back to top button