Burudani

Tom Holland kuigiza na Sabrina Carpenter

NEW YORK: MWIMBAJI na mwigizaji maarufu wa Marekani, Sabrina Carpenter, anatarajiwa kuigiza pamoja na nyota wa filamu Tom Holland katika filamu mpya inayomzungumzia mwanamuziki na mcheza dansi maarufu wa Hollywood, Fred Astaire.

Carpenter atacheza nafasi ya Ginger Rogers, mwigizaji na mcheza dansi aliyekuwa mshirika maarufu wa Fred Astaire katika filamu kadhaa za Hollywood.

Tom Holland, anayefahamika zaidi kwa nafasi yake ya Spider-Man, atacheza nafasi ya Fred Astaire katika filamu hiyo ambayo bado haijapewa jina rasmi. Margaret Qualley naye atacheza nafasi ya Adele Astaire, dada wa Fred na mshirika wake wa awali katika dansi.

Filamu hiyo itaongozwa na Paul King, anayefahamika kwa kuongoza filamu za ‘Paddington’ na ‘Wonka’, huku simulizi ikitokana na kitabu The Astaires: Fred & Adele kilichoandikwa na Kathleen Riley.

Kwa upande wa Carpenter, ujio wake katika filamu hiyo unaendelea kuonesha upande wake wa uigizaji mbali na muziki, huku akichukua nafasi ya mwanamke aliyekuwa sehemu muhimu ya historia ya Fred Astaire huko Hollywood.

Holland naye tayari ameanza maandalizi ya kucheza nafasi hiyo, huku akirejea katika dansi baada ya uzoefu wake wa awali kwenye jukwaa la Billy Elliot the Musical nchini Uingereza.

Related Articles

Back to top button