Burudani

Mchekeshaji aacha sigara baada ya kunyimwa busu na mkewe

NAIROBI, Kenya: MCHEKESHAJI na mtayarishaji wa maudhui nchini Kenya, Terence Creative, anayefahamika pia kwa jina lake halisi Lawrence Macharia, ameadhimisha miaka tisa na siku 26 tangu aache matumizi ya sigara na aina nyingine za uvutaji wa kilevi.

Terence, maarufu kwa vichekesho vyake vya ‘Wash Wash’ na ushiriki wake katika kipindi cha Churchill Show, alieleza kupitia mitandao ya kijamii kuwa awali alikuwa na uraibu mkubwa wa sigara, ambapo alikuwa akivuta hadi sigara 60 kwa siku, sawa na pakiti tatu, pamoja na kutumia shisha na bangi.

Alisema tabia hiyo ilikuwa imeathiri afya na mwonekano wake kwa kiasi kikubwa, akipata matatizo ya kupumua, fizi kuvuja damu, harufu mbaya ya mwili na hali ya kuonekana mchovu.

Katika simulizi yake, Terence pia alifichua namna uraibu huo ulivyoathiri uhusiano wake na mkewe, Milly Chebby, ambaye alimuwekea sharti la kuacha kabisa uvutaji kabla ya kumruhusu kumbusu kimapenzi.

Kwa mujibu wa simulizi hiyo, Milly alidumisha msimamo huo kwa miaka sita, jambo lililokuwa sehemu ya changamoto alizokutana nazo Terence katika uhusiano wao.

Wawili hao walifahamiana walipokuwa wakifanya kazi katika kipindi cha Churchill Show, ambapo Milly alikuwa msimamizi wa shughuli za nyuma ya jukwaa huku Terence akiwa mwandishi na mchekeshaji.

Terence amesema uamuzi wa kuacha sigara, shisha na bangi umekuwa hatua muhimu katika maisha yake, huku akiadhimisha miaka tisa bila kuvuta chochote yakionesha safari yake ya kujinasua kutoka kwenye uraibu huo.

Related Articles

Back to top button