Muziki

Paul McCartney awa mwanamuziki wa tatu tajiri duniani

LONDON: MWANAMUZIKI mkongwe wa Uingereza na aliyekuwa mwanachama wa bendi ya The Beatles, Sir Paul McCartney, amejiunga na orodha ya mabilionea duniani baada ya utajiri wake kukadiriwa kufikia dola bilioni 1.4 ni takribani shilingi trilioni 3.7 za Tanzania (TSh 3,703,000,000,000). kwa mujibu wa Forbes.

McCartney, mwenye umri wa miaka 84, sasa anatajwa kuwa mwanamuziki wa tatu tajiri zaidi duniani, akiwafuata Jay-Z mwenye utajiri wa dola bilioni 2.8 na Taylor Swift anayekadiriwa kuwa na dola bilioni 2. Utajiri wake unatokana zaidi na haki za muziki, biashara ya uchapishaji wa nyimbo na ziara mbalimbali za kimataifa.

Mwaka 1969, McCartney alianzisha kampuni yake ya uchapishaji wa muziki, MPL Communications, baada ya kutoridhishwa na mikataba ya awali ya The Beatles. Kampuni hiyo kwa sasa inamiliki haki za maelfu ya nyimbo, zikiwemo kazi zake binafsi na nyimbo maarufu za wasanii wengine.

Aidha, sehemu yake ya mapato kutoka katalogi ya nyimbo za Lennon-McCartney inakadiriwa kumuingizia angalau dola milioni 10 kwa mwaka. Kampuni ya The Beatles pia hupata zaidi ya dola milioni 50 kila mwaka kupitia huduma za utiririshaji wa muziki, mauzo ya santuri na bidhaa mbalimbali, huku McCartney akipokea asilimia 25 ya mapato hayo.

Mbali na muziki, utajiri wake unajumuisha majengo ya thamani nchini Uingereza na eneo la Hamptons nchini Marekani, pamoja na mkusanyiko wa sanaa wenye kazi za wasanii maarufu kama Pablo Picasso na René Magritte.

McCartney pia amejipatia mamilioni ya fedha kupitia matamasha ya moja kwa moja. Kati ya mwaka 2022 na 2025, alikamilisha jumla ya maonesho 79 katika ziara yake ya dunia ya ‘Got Back’, hatua inayodhihirisha mchango wa muziki na maonesho katika kukuza utajiri wake.

Related Articles

Back to top button