Beckham kuingizwa Ukumbi wa Mastaa wa Soka Marekani

LONDON: NYOTA wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya England, David Beckham, anatarajiwa kuingizwa kwenye Ukumbi wa Umaarufu wa Soka Marekani (National Soccer Hall of Fame) katika kundi la mwaka 2027.
Beckham, mwenye umri wa miaka 51, alijiunga na LA Galaxy mwaka 2007 akitokea Real Madrid ya Hispania kwa mkataba wa miaka mitano.
Katika kipindi chake cha misimu sita, alicheza mechi 124 na kufunga mabao 20, huku akiisaidia klabu hiyo kutwaa mataji mawili ya MLS Cup na mawili ya Supporters’ Shield.
Mchango wake ulisaidia kuongeza umaarufu wa Ligi ya Soka Marekani (MLS) kimataifa. Baada ya kustaafu mwaka 2013, Beckham aliendelea kujihusisha na soka kwa kuwa mmiliki mwenza wa klabu ya Inter Miami, iliyomsajili nyota wa Argentina, Lionel Messi, mwaka 2023.
Sherehe za kumuingiza kwenye ukumbi huo zinatarajiwa kufanyika Aprili 16, 2027, jijini Frisco, Texas. Beckham alielezwa kuhusu kuchaguliwa kwake kupitia kura ya kundi la wachezaji wa zamani na kueleza kuwa kipindi chake nchini Marekani kilikuwa safari ya kipekee, huku akiahidi kuendelea kuchangia maendeleo ya soka nchini humo.
Mbali na Beckham, nyota wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake ya Marekani, Megan Rapinoe na Julie Ertz, nao wamechaguliwa kuingia kwenye ukumbi huo katika mwaka wao wa kwanza.
Wawili hao walikuwa sehemu ya kikosi cha Marekani kilichotwaa Kombe la Dunia la Wanawake mwaka 2015 na 2019.
Rapinoe, mwenye umri wa miaka 41, alieleza kuwa kutambuliwa pamoja na wachezaji wakubwa walioitumikia nchi yake ni heshima kubwa na ishara ya mafanikio waliyoyapata wakiwa sehemu ya timu bora.



