Bien ahisiwa kufanya collabo na msanii wa Marekani Muni Long

HOLLYWOOD, Marekani: MWANAMUZIKI maarufu kutoka Kenya, Bien-Aimé Baraza, amezua gumzo miongoni mwa mashabiki wa muziki baada ya kuonekana akiwa pamoja na mwimbaji wa R&B kutoka Marekani, Muni Long, jijini Hollywood, hali iliyochochea tetesi za uwezekano wa kufanya kazi ya pamoja kimuziki.
Mkutano huo umeibua maswali kuhusu uwezekano wa wasanii hao kuandaa wimbo wa pamoja, ingawa hakuna kati yao aliyethibitisha kuwa kuna mradi wowote wa muziki unaoendelea.
Bien, ambaye ni mwanachama wa zamani wa kundi la Sauti Sol, amekuwa akipanua wigo wake wa muziki nje ya Kenya kupitia kazi na shughuli mbalimbali za kimataifa.
Kwa upande wake, Muni Long anafahamika kupitia nyimbo zake za R&B pamoja na uwezo wake wa kuandika nyimbo.
Kukutana kwake na Bien kumeongeza matarajio miongoni mwa mashabiki wa Kenya wanaotamani kuona mwanamuziki huyo akifanya kazi na wasanii wakubwa wa kimataifa.
Hata hivyo, mazungumzo yao yamekuwa sehemu nyingine ya mjadala mitandaoni, ambapo baadhi ya mashabiki walijikita katika lugha iliyotumika wakati wa mawasiliano yao. Baadhi walitania kuwa Bien alionekana kuzungumza Kiswahili badala ya Kiingereza.
Shabiki mmoja aliyetambulika kwa jina la aaron_amby aliandika, “Lakini Bien alitaka muongee Kiswahili, mwamba ukagoma,” huku mwingine akitoa maoni kuwa Bien alionekana kuwa huru zaidi kuwasiliana kwa Kiswahili.
Licha ya gumzo hilo, mashabiki wanasubiri kuona kama kukutana kwa wasanii hao kutazaa ushirikiano wa kimuziki utakaomfungulia Bien milango zaidi katika soko la muziki wa kimataifa.




