Timu ya Taifa ya Kenya yaibugiza Lesotho mabao 6-0

LUSAKA: TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Kenya, Harambee Starlets, imeonesha ubora mkubwa baada ya kuichapa Lesotho mabao 6-0 katika mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON).
Nyota wa mchezo huo alikuwa Eglay Mukhwana aliyefunga mabao mawili huku Violet Nanjala, Terry Engesha, Fasila Adhiambo na Catherine Khaemba wakifunga mabao mengine.
Kenya ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kwanza dakika ya 11 kupitia Violet Nanjala kabla ya Terry kuongeza la pili dakika ya 14. Fasila Adhiambo aliifungia Kenya bao la tatu dakika ya 27 huku Mukhwana akifunga la nne kabla ya mapumziko.
Kipindi cha pili, Mukhwana aliongeza bao la tano dakika ya 65 kabla ya Catherine Khaemba kufunga bao la sita dakika ya 74 na kuhitimisha ushindi mnono wa Starlets.
Kocha Beldine Odemba aliisifu timu yake kwa kuonesha kiwango kizuri na kutumia mchezo huo kuwapima wachezaji wake kuelekea mashindano yajayo ya kimataifa.



