Africa

Taifa Stars, Madagascar kusaka ushindi Morocco

CASABLANCA: TAIFA Stars leo itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Madagascar katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Stade de Houener nchini Morocco kuanzia saa 11:00 jioni, huku timu zote zikiingia uwanjani zikisaka ushindi baada ya kupoteza michezo yao iliyopita.

Taifa Stars, chini ya Kocha Mkuu Miguel Gamondi, ilipoteza mchezo wake uliopita kwa kufungwa mabao 2-0 na Guinea-Bissau katika mchezo uliochezwa Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, hivyo itakuwa na kazi ya kurejea kwenye ushindi mbele ya Madagascar.

Madagascar nayo inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza dhidi ya Nigeria kwa mabao 2-1, hali inayofanya mchezo wa leo kuwa muhimu kwa timu zote mbili katika kutafuta matokeo mazuri.

Gamondi amesema maandalizi ya timu hayakuwa ya muda mrefu kutokana na safari kutoka Tanzania kwenda Morocco, lakini amesisitiza kuwa kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo baada ya kufanya mazoezi mepesi na kutathmini hali za wachezaji.

“Madagascar ni timu nzuri. Tumeiona ilivyocheza dhidi ya Nigeria na tunatarajia mchezo mgumu. Tunahitaji kutathmini wachezaji wote walio katika hali nzuri na huenda tukafanya mabadiliko ili kuwapa nafasi wachezaji waliopo kwenye kundi,” amesema Gamondi.

Kocha huyo amesema licha ya changamoto ya maandalizi, lengo la Stars ni kufanya vizuri na kuwa na ufanisi zaidi mbele ya lango ili kupata mabao.

Kwa upande wake, nahodha wa kikosi hicho Simon Msuva amesema kikosi hicho kimefika salama Morocco na maandalizi yamefanyika vizuri licha ya kuwa na muda mfupi.

“Mchezo wetu wa kesho (leo) dhidi ya Madagascar ni muhimu. Madagascar ni timu nzuri, tunaiheshimu na tumeshacheza nayo zaidi ya mara moja. Nipo hapa kuhakikisha tunafanya vizuri na wachezaji wote tupo tayari kukabiliana nao,” amesema Msuva.

Msuva amesema Stars haina sababu ya kutoa visingizio, akisisitiza kuwa wachezaji wako tayari kupambana ili kupata ushindi na kuwataka Watanzania kuendelea kuwaombea na kuwa na imani na timu.

Tanzania na Madagascar zimekutana mara kadhaa, huku mchezo wao wa mwisho katika michuano ya CHAN mwaka 2025 ukimalizika kwa Stars kushinda mabao 2-1. Hata hivyo, katika michuano ya COSAFA, Tanzania ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Madagascar.

Stars sasa inahitaji kutumia uzoefu huo pamoja na maandalizi yaliyofanyika Morocco kuhakikisha inapata matokeo mazuri katika mchezo huo wa leo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button