Mwana FA: Jeshi limetekeleza maelekezo ya Rais
NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ amefungua Mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi ambapo amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) hususani Mkuu wa Majeshi nchini, Jenerali Jacob Mkunda kwa kuja na wazo la kuwa na mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi (CDF Cultural Competition).
Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa mashindano hayo Msasani Beach Jijini Dar es salaam Mwinjuma amesema Jeshi limetekeleza kwa vitendo maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu kuwa kila mmoja ana wajibu wa kupenda, kuenzi na kuendeleza utamaduni wetu.
“Nimefurahi sana kusikia kuwa mashindano haya yatakuwa yanafanyika kila mwaka lakini kwa mwaka huu ni sehemu ya shamrashamra za kusherehekea miaka 60 ya Jeshi letu. Jambo hili ni la msingi sana kwa uhai wa taifa letu na ukweli Jeshi limeandika historia kubwa ”
Mwana FA ameonesha kupendezwa na mwamko wa vikundi vya sanaa vya Jeshi kushiriki mashindano hayo pia ambavyo jeshi limeweza kuwa na bendi na vikundi vya ngoma vingi ambavyo kipekee vinadumisha na kuendeleza utamaduni.
“Kufanyika kwa mashindano haya kwetu imekuwa ni faraja kubwa, niahidi hapa kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk.Damas Ndumbaro kuwa Wizara itatoa kila aina ya msaada unaotakiwa kuhakikisha mashindano haya muhimu yanafanikiwa”amesema Mwana FA