Wema Sepetu: Nimepata ujauzito kwa njia ya kawaida, ‘Only God’

DAR ES SALAAM: MSANII na mwigizaji maarufu nchini, Wema Sepetu, amefunguka kuhusu ujauzito wake na kusema amefanikiwa kupata ujauzito kwa njia ya kawaida bila kutumia teknolojia ya IVF.
Wema ametoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram baada ya kuulizwa na mashabiki kuhusu namna alivyofanikiwa kupata ujauzito huo baada ya kusubiri kwa muda mrefu.
Akijibu swali la shabiki aliyetaka kujua alikofanyia IVF, Wema alionesha kushangazwa na dhana hiyo na kusisitiza kuwa kwake jambo hilo limetokea kwa uwezo wa Mungu.
“Jamani… Hivi kumbe kuna watu hawaamini Mungu ee… Nilishasema na nikaapa kwamba kama haitatokea kawaida sitohangaika maana kukata tamaa nilishakata muda… Aaaah nimechoka sasa…!!! IVF ya kazi gani…?” ameandika Wema.
Katika jibu jingine, Wema alisema kwa ufupi, “Only God hun… Only God.”
Kauli hiyo imeendelea kuzua mjadala mitandaoni, huku mashabiki wengi wakimpongeza kwa hatua hiyo na kueleza furaha yao baada ya muda mrefu wa kusubiri kwake kutimiza ndoto ya kuwa mama.
Kwa miaka kadhaa, Wema amekuwa akizungumza kuhusu hamu yake ya kupata mtoto, jambo lililofanya taarifa za ujauzito wake kupokelewa kwa furaha kubwa na mashabiki pamoja na wadau wa burudani.
Kwa sasa, mashabiki wake wanaendelea kufuatilia kwa karibu safari yake ya ujauzito huku wakimtakia afya njema na kila la heri katika hatua hii mpya ya maisha yake.




