Simba yaifuata Singida BS kibabe

SINGIDA: Simba imetua mkoani Singida kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Black Stars unaotarajiwa kuchezwa Jumatano ya wiki hii kwenye Uwanja wa Airtel.
Akizungumza na SpotiLeo, Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, amesema wanautambua ugumu wa mchezo huo lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
“Tunajua tunakwenda kucheza na timu imara ambayo ipo nyumbani na ina wachezaji wazuri, hivyo hatutarajii mchezo mwepesi. Lakini sisi kama Simba tumefanya maandalizi mazuri na kikosi kipo tayari kwa ajili ya kupambana na kuhakikisha tunapata matokeo chanya,” amesema Ahmed.
Amesema kila mchezo kwao ni muhimu hivyo wataingia uwanjani kwa umakini mkubwa ili kutimiza malengo ya timu.
“Tunaiheshimu Singida Black Stars kwa sababu imekuwa ikifanya vizuri, lakini sisi pia tunajua thamani ya alama tatu katika hatua hii ya ligi, hivyo mashabiki wategemee kuona timu ikipambana kwa nguvu zote,” ameongeza.
Hata hivyo, Singida Black Stars kupitia kwa Msemaji wake Hussein Masanza amesema mchezo huo una hadhi kubwa na unatarajiwa kuwa mchezo wenye ushindani.
“Ni mchezo wenye hadhi kubwa ya kitaifa kwa sababu unazikutanisha timu mbili zenye ushindani mkubwa. Simba ni timu ambayo imeimarika sana, hivyo tunaamini utakuwa mchezo mzuri na wenye ushindani mkubwa kwa mashabiki,” amesema Masanza.




