Neymar avunja rekodi ya Pelé
FOWADI Neymar da Silva Santos Júnior, Neymar Jr amempiku Edson Arantes do Nascimento maarufu Pelé, kwa ufungaji mabao Brazil alipofunga mabao mawili katika ushindi wa 5-1 dhidi ya Bolivia.
Nyemar mwenye umri wa 31, ambaye aliingia katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia akiwa sawa na Pelé kwa idadi ya mabo 77 alikosa penalti kabla ya kufunga mawili ikiwa ni mchezo wake wa 125 timu ya taifa Brazil.
“Sikuwahi kufikiria kufikia rekodi hii. Mimi si bora kuliko Pelé au mchezaji mwingine yeyote wa timu ya taifa,” amesema Neymar Jr.
Pelé, ambaye alifariki dunia Desemba 2022 akiwa na umri wa miaka 82, alifunga mabao 77 katika michezo 92 kati ya mwaka 1957 na 1971.
Anachukuliwa kuwa mmoja wa wanasoka bora zaidi kuwahi kucheza soka.
Ukurasa rasmi wa Pelé katika mtandao wa kijamii wa X umepongeza mafanikio hayo ya Neymar.
“Hongera Neymar kwa kumpiku Mfalme kwa mabao Brazil. Hakika leo Pelé anakupongeza!,” umesema.
Kocha wa Brazil Fernando Diniz amesema : “Alikuja kufanya kile alichofanya: kufurahia, kufunga mabao mawili na kuvunja rekodi.”
Neymar alikuwa mchezaji ghali zaidi duniani alipojiunga na Paris Saint-Germain kutoka Barcelona mwaka 2017 kwa ada ya pauni milioni 200 sawa na shilingi bilioni 610.
Aliondoka klabu hiyo ya Ufaransa majira ya kiangazi kujiunga na timu ya Al-Hilal inayoshiriki Ligi ya Kulipwa ya Saudi Arabia.