Gamondi: Kesho mtaona mabadiliko makubwa

KOCHA Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amewaahidi mashabiki wa soka matokeo mazuri wakati klabu itakapoikabili Asas Djibouti Agosti 20 katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Amesema hayo leo Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
“Kitu muhimu zaidi kwenye mchezo ni kufunga magoli, tumejiandaa na tumelifanyia kazi hilo na ninaamini kesho mtaona mabadiliko makubwa kwenye eneo hilo,” amesema Gamondi.
Gamondi amesema wachezaji wanakwenda kuiwakilisha Yanga na Tanzania kwa ujumla, hivyo anaamini watakuwa na mchezo mzuri na kuwa na mwanzo mzuri kwenye Ligi ya Mabingwa.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wengine beki wa kushoto wa Yanga, Nickson Kibabage amesema watakuwa makini katika mchezo huo na kufanyia kazi maelekezo ya kocha.
“Hatudharau mpinzani. Unapokutana na mpinzani kwenye Ligi ya Mabingwa bila shaka anakuwa amefanya vizuri alipotoka, tutakwenda kwa umakini mkubwa na kufanyia kazi yale ambayo kocha ametuelekeza,” amesema Kibabage.
Mchezo wa marudiano kati ya timu hizo utafanyika Agosti 26 kwenye uwanja huo huo wa Azam Complex.