Africa

Patel akaribia ubingwa wa Afrika wa mashindano ya magari

RWANDA: Dereva wa magari ya mashindano kutoka Kenya, Karan Patel, amesema ana imani kubwa ya kutimiza ndoto yake ya kutwaa ubingwa wa Mashindano ya Afrika ya Magari ya Mbio (FIA African Rally Championship – ARC) mwaka 2026 baada ya kuibuka mshindi katika mashindano ya Mountain Gorilla Rally yaliyofanyika nchini Rwanda.

Ushindi huo, ambao ni wa nne kwa Patel katika Rally ya Rwanda, umeimarisha nafasi yake kileleni mwa msimamo wa ARC akiwa na jumla ya alama 118. Mafanikio hayo yamempa alama kubwa dhidi ya wapinzani wake huku mashindano yakifikia nusu ya msimu.

Akizungumza baada ya ushindi huo, Patel alisema matokeo hayo yameongeza imani kwake na kwa timu yake kwamba wana uwezo wa kutwaa ubingwa wa Afrika msimu huu. Alikiri kuwa msimu uliopita ulikuwa na changamoto nyingi, lakini walifanikiwa kuumaliza kwa kiwango kizuri nchini Tanzania, jambo lililowapa nguvu ya kuanza vyema kampeni ya mwaka huu.

“Mwaka jana tulipitia nyakati ngumu, lakini tulimaliza msimu vizuri Tanzania. Hilo lilitupa morali kwa msimu huu ambao umekuwa mzuri sana hadi sasa. Hakuna kilicho na uhakika, lakini tutaendelea kupambana kwa sababu ndoto yangu ni kuwa bingwa wa Afrika,” alisema Patel.

Akiwa na msaada wa msomaji ramani wake wa muda mrefu, Tauseef Khan, Patel alitawala mashindano hayo kwa kushinda hatua maalumu 10 kati ya 12 zilizochezwa katika maeneo ya Kigali na Bugesera, akionyesha ubora wake na kuthibitisha kuwa ndiye mgombea mkuu wa ubingwa wa mwaka huu.

Kwa sasa Patel anaongoza msimamo wa ARC akiwa na alama 118, akifuatiwa na Mkenya mwenzake Aakif Virani mwenye alama 85. Nafasi ya tatu inashikiliwa na Jasmeet Chana mwenye alama 67, huku Samman Vohra akiwa wa nne na alama 66. Nikhil Sachania yuko nafasi ya tano akiwa na alama 56, wakati Mhindi Naveen Puligilla amepanda hadi nafasi ya sita akiwa na alama 39.

Mashindano yajayo ya ARC yatafanyika Tanzania kupitia Mkwawa Rally kuanzia Oktoba 2 hadi 4. Patel ana rekodi nzuri katika mbio hizo baada ya kushinda mwaka 2022 na 2025 akiwa anaendesha gari aina ya Škoda Fabia Rally2 evo, na sasa atalenga kuendeleza ubabe wake ili kusogea karibu zaidi na kutwaa taji la kwanza la ubingwa wa Afrika.

Related Articles

Back to top button