Deschamp akiaga, Mbappe akiwinda rekodi mechi nafasi ya tatu

MAREKANI: Ufaransa na England zitashuka dimbani Jumamosi mjini Miami kuwania nafasi ya tatu ya Kombe la Dunia 2026, katika mechi ambayo licha ya kutokuwa na uzito wa fainali, imebeba simulizi mbili kubwa; kuaga kwa heshima kwa kocha Didier Deschamps na harakati za Kylian Mbappe kuweka rekodi mpya ya mabao katika historia ya Kombe la Dunia.
Timu zote mbili zinaingia kwenye mchezo huo zikiwa na maumivu ya kutolewa kwenye hatua ya nusu fainali. Ufaransa ilifungwa mabao 2-0 na Hispania, huku England ikipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya mabingwa watetezi Argentina baada ya kushindwa kulinda bao lao la kuongoza.
Kwa Deschamps, mchezo huo utakuwa wa mwisho kuinoa timu ya taifa ya Ufaransa baada ya kuitumikia kwa miaka 14. Katika kipindi hicho, aliiongoza Les Bleus kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2018, kufika fainali mwaka 2022 na kutinga hatua ya nusu fainali mara tatu mfululizo, mafanikio yaliyomweka miongoni mwa makocha bora katika historia ya soka la Ufaransa.
Kwa upande wa Mbappe, nyota huyo ana nafasi ya kuandika historia nyingine katika mashindano hayo. Akiwa amefunga mabao nane kwenye Kombe la Dunia 2026 na kufikisha mabao 20 kwa jumla katika historia ya michuano hiyo, mshambuliaji huyo anawania Kiatu cha Dhahabu pamoja na kuvunja rekodi ya mabao mengi zaidi katika Kombe la Dunia.
Kutokana na uchovu wa kimwili na kisaikolojia baada ya safari ndefu ya mashindano, inatarajiwa makocha wote wawili wafanye mabadiliko makubwa katika vikosi vyao kwa kuwapa nafasi wachezaji ambao hawakupata muda mwingi wa kucheza. Kocha wa England Thomas Tuchel amesema hakuna mchezaji aliyekuwa na ndoto ya kucheza mechi ya nafasi ya tatu, kwani lengo lao lilikuwa kufika fainali.
Licha ya kupungua kwa presha ya ushindi wa ubingwa, mchezo huo bado una umuhimu mkubwa kwa wachezaji wanaotafuta kuthibitisha uwezo wao, huku Mbappe akisaka historia na Deschamps akitafuta kuhitimisha enzi yake kwa ushindi. Hivyo, mechi ya medali ya shaba inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa licha ya kutokuwa fainali ambayo timu zote mbili zilikuwa zikiitamani.




