Olimpiki ya Paris iliupamba mwaka 2024

MICHEZO ya Olimpiki ni mashindano makubwa ya michezo mbalimbali duniani inayofanyika kila baada ya miaka minne.
Kwa mwaka 2024 mashindano hayo makubwa yalifanyika katika jiji la Paris nchini Ufaransa ambapo wanariadha kutoka zaidi ya nchi 200 walishiriki kugombea medali 329 katika michezo 32 kwenye mashindano yote.
Michezo ya Olimpiki imekuwa na historia ndefu katika vipindi viwili ikiwemo michezo ya Olimpiki ya Kale na Kisasa:
Michezo ya Olimpiki ya Kale ilifanyika kuanzia mwaka 776 KK hadi mwaka 393 BK katika mtaa wa mahekalu wa Olimpia kwenye rasi ya Peloponesi nchini Ugiriki.
Madhumuni ya michezo hiyo ilikuwa ni tamasha la kidini, kumtukuza Zeus ambaye alikuwa Mfalme wa miungu nchini humo na ilikuwa inafanyika kila baada ya miaka minne. Wakati huo, watu wote nchini Ugiriki walishiriki kwa pamoja katika tamasha hilo mbele ya Mfalme huyo.
Lakini Historia ya Michezo ya Olimpiki ya Kisasa inaelezwa ilianza mwaka 1896 mjini Athens nchini Ugiriki. Mwanzilishi alikuwa Mfaransa Pierre de Coubertin aliyetaka kutumia michezo ya kale kwa kujenga uhusiano mzuri kati ya vijana wa nchi mbalimbali na kuwapatia nafasi ya kushindana kwenye uwanja wa michezo badala ya uwanja wa vita.
Mwaka huo wa 1896, wanamichezo 280 wote wakiwa wanaume kutoka mataifa 13 walishiriki katika michezo 43 iliyochezwa katika tamasha hilo.
Kutokana na wazo bilo Coubertin alianzisha Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (International Olympic Committee – IOC) ili kuendesha michezo hiyo na kutoa zawadi kwa washindi watatu kwa kila mchezo ambapo Michezo hii ya kisasa imeendelea kila baada ya miaka minne isipokuwa 1916, 1940 na 1944 kwa sababu ya Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia.
Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 ya Majira ya joto ilifanyika kwenye Uwanja wa Stade de France kwa zaidi ya siku 15, ilianza Julai 26 hadi Agosti 11 ambapo karibu wanariadha 11,000 walishindana katika mbio na michezo mbalimbali kwa lengo la kupata medali mbalimbali.
Takriban wanariadha 9,000 waliofurika katika uzinduzi wa michezo hiyo kutoka mataifa mbalimbali waliburudishwa na wasanii 270, watazamaji katika Michezo hiyo Uwanjani walikuwa takribani 71,500, katika uwanja wa Stade de France.
Wanariadha kutoka zaidi ya nchi 200 wameshindania medali 329 katika michezo 32 kwenye mashindano yote ilyochezwa katika mashidano hayo.
Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 baada ya kufungwa imekabidhi kijiti kwa Jiji la Los Angeles nchini Marekani kwa ajili ya michezo hiyo itakayofanyika mwaka 2028, imeashiria mwanzo wa miaka minne ya maandalizi kuelekea jiji hilo ambapo mwanariadha wa Marekani Simone Biles alijiunga na meya wa Los Angeles, Karen Bass wakati bendera ya Olimpiki ilipokabidhiwa rasmi kwao.
Marekani ambayo ndiyo itakayoandaa mashindano ya Olimpiki yajayo ya Los Angeles 2028 ndiyo nchi iliyoondoka na medali nyingi zaidi kuliko nchi nyingine zilizoshiriki katika mashindano hayo ya Paris 2014.
Marekani ilijinyakulia tuzo 40 za Dhahabu, Fedha 44 na Shaba 42 ikiwa imeshinda jumla ya medali 126.
China ndiyo iliyoshika nafasi ya pili ikijizolea medali 91 zikiwemo dhahabu 40, fedha 27 na shaba 21. Japan ilishika nafasi ya tatu ikijinyakulia jumla ya tuzo 45 zikiwemo dhahabu 20, fedha 12 na shaba 13.
Australia ilishika nafasi ya nne ikijizolea jumla ya medali 53 zikiwemo dhahabu 18, fedha 19 na shaba 16 na Ufaransa ambayo ndiyo waandaaji wa mashindano hayo ilijizolea jumla ya medali 64 ikawa nafasi ya tano ikiwa na dhahabu 16, fedha 26 na shaba 22.
Kwa nchi za Afrika Kenya imeshika nafasi ya 1 na 17 kwa nchi zote zilizoshiriki mashindano hayo ikiwa na jumla ya medali 11 huku Dhahabu zikiwa 4, Fedha 2 na Shaba 5. Afrika Afrika Kusini imeshika nafasi ya 2 na 44 kwa nchi zote zilizoshiriki mashindano hayo ikiwa na jumla ya medali 6 huku dhahabu 1, fedha 3 na shaba 2.
Ethiopia imeshika nafasi ya 3 na 47 kwa nchi zote zilizoshiriki mashindano hayo ikiwa na jumla ya medali 4 huku dhahabu 1 na fedha 3. Uganda ya 2 kwa Afrika Mashariki na ya 4 kwa Afrika huku ikishika nafasi ya 55 kati ya nchi zote zilizoshiriki mashindano hayo Paris 2024 ikiwa na jumla ya medali 2, dhahabu 1 na fedha 1 haina shaba.
Morocco ya ni ya tano kwa Afrika na ya 60 kati ya nchi zote zilizoshiriki mashindano hayo Paris 2024 ikiwa na jumla ya medali 2, Dhahabu 1 na Shaba 1. Zambia ilishika nafasi ya 6 kwa Afrika na 84 kwa dunia ikiwa na medali 1 tu ya shaba. Tanzania haikuambulia kiti katika mashindano hayo ya Paris 2024.