Africa

Okello atua Far Rabat akutana na kocha Gonçalves

MOROCCO: Kiungo mshambuliaji wa Uganda, Allan “Star Boy” Okello, amekamilisha uhamisho wake kutoka klabu ya Tanzania, Young Africans (Yanga SC), kwenda AS FAR Rabat ya Morocco. Klabu hiyo imemtambulisha rasmi Okello baada ya kukamilika kwa makubaliano ya uhamisho.

Okello, mwenye umri wa miaka 26, amejiunga na AS FAR Rabat kwa mkataba wa miaka mitatu, akianza sura mpya ya maisha yake ya soka nchini Morocco. Uhamisho huo unamrudisha katika soka la Afrika Kaskazini baada ya awali kucheza nchini Algeria.

Mchezaji huyo ameondoka Yanga baada ya kuwa na kipindi kifupi lakini chenye mafanikio tangu alipojiunga na mabingwa hao wa Tanzania. Katika kipindi chake, Okello alionesha uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi na kufunga mabao, jambo lililovutia klabu kutoka Morocco.

AS FAR Rabat ni miongoni mwa klabu kubwa nchini Morocco na imekuwa ikishiriki mashindano ya kimataifa ya CAF. Msimu uliopita, klabu hiyo ilifika hadi fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo ujio wa Okello unaipa nafasi ya kucheza katika mazingira ya ushindani mkubwa zaidi barani Afrika.

Kwa upande wa Okello, uhamisho huo ni hatua nyingine muhimu katika safari yake ya kimataifa, baada ya kucheza Uganda, Algeria na Tanzania. Pia atakuwa akifanya kazi tena chini ya kocha Pedro Gonçalves, ambaye aliwahi kufanya kazi naye wakati akiwa Yanga.

Akizungumza baada ya kujiunga na klabu hiyo, Okello amesema ana furaha kujiunga na AS FAR Rabat na ameahidi kufanya kila awezalo kuisaidia timu hiyo kushinda mataji. “Ninafuraha sana kujiunga na timu kubwa kama AS FAR. Ninaahidi kufanya kila niwezalo kuisaidia timu kushinda mataji,” amesema Okello.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button