Kwingineko

Mourinho atoa msimamo mkali Madrid

MADRID:KOCHA mpya wa Real Madrid, Jose Mourinho, ameanza safari yake ya pili katika klabu hiyo kwa msimamo mkali, akisisitiza kuwa maslahi ya timu lazima yawe mbele ya hisia binafsi za wachezaji.

Mourinho ametoa kauli hiyo katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari leo tangu kurejea Real Madrid, siku chache kabla ya mchezo wao wa kwanza wa LaLiga dhidi ya Espanyol.

Kocha huyo amesema ushindani wa nafasi ndani ya kikosi ni jambo lisiloepukika, hivyo wachezaji hawapaswi kukata tamaa au kulalamika wanapokosa nafasi ya kucheza, bali wanapaswa kuongeza juhudi ili kuonesha wanastahili kuanza.

“Ahadi na kujituma ni lazima. Timu lazima iwe mbele ya hisia binafsi. Sitaki wachezaji wanaonaswa na hasira au kukata tamaa kwa sababu hawakucheza, nataka wale wanaofanya kazi kwa bidii zaidi ili kupata nafasi,” amesema Mourinho.

Mourinho pia amekiri kuwa atakuwa na kazi kubwa ya kuwapanga kwa pamoja nyota Kylian Mbappé, Jude Bellingham na Vinícius Júnior, akisema ni vigumu kujenga timu inayomzunguka kila mmoja wao kama ilivyo katika timu zao za taifa.

Hata hivyo, amesema anaamini wachezaji hao wanaweza kucheza pamoja na kuisaidia Real Madrid kuwa na msimu mzuri.

Katika hatua nyingine, Mourinho amesema ameamua kuanza upya uhusiano wake na viungo Aurelien Tchouameni na Federico Valverde, baada ya wawili hao kuhusishwa na ugomvi wa vyumba vya kubadilishia nguo mwishoni mwa msimu uliopita.
Amesema alichokiona tangu kuanza kwa maandalizi ni hali ya kawaida, urafiki na ushirikiano kati yao, hivyo haoni sababu ya kuendelea kulizungumzia suala hilo.

Real Madrid inaingia msimu mpya ikiwa imetoka katika misimu miwili mfululizo bila kutwaa taji, jambo linaloongeza presha kwa Mourinho kurejesha mafanikio katika klabu hiyo.

Related Articles

Back to top button