Odemba: Kujipromoti si kujisifu, kujituma si kujikweza

DAR ES SALAAM: MREMBO na Mwanamitindo wa kimataifa, Miriam Odemba, amesema anafurahia ushindi wa Jihan Dimack aliyetwaa taji la Miss Grand International 2026, huku akisisitiza kuwa kujipromoti si kujisifu, kujituma si kujikweza na kujiamini si kujiona bora kuliko wengine.
Odemba ameyasema hayo kupitia machapisho kadhaa aliyoweka kwenye ukurasa wake wa Instagram, akijibu maoni ya baadhi ya mashabiki waliohoji machapisho yake yaliyofuatia ushindi wa Jihan.
Baadhi ya mashabiki walitafsiri machapisho hayo kama njia ya Odemba kujitangaza upya, baada ya kushiriki kumbukumbu za mafanikio yake ya zamani, ikiwemo kushika nafasi ya pili katika mashindano ya Miss Earth mwaka 2008.
Machapisho hayo pia yalihusisha picha za Jihan pamoja na warembo wengine wa Tanzania waliowahi kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ya urembo.
Hata hivyo, baadhi ya mashabiki walitoa maoni kuwa, licha ya mafanikio ya Odemba katika miaka iliyopita, wakati huo ulikuwa wa Jihan kupongezwa na kufurahia ushindi wake bila kuhusisha mafanikio ya wengine.
Akijibu maoni hayo, Odemba amesisitiza kuwa anathamini ushindi wa Jihan, huku akieleza kuwa kujitangaza na kuonesha mafanikio yake si sawa na kujisifu au kujiona bora kuliko wengine.
Odemba amesema anaamini katika kufanya kazi kwa bidii, kujitangaza, kujifunza na kusimama imara katika kile anachokiamini.
Ameongeza kuwa haoni sababu ya kukaa pembeni na kusubiri watu wamgundue, wakati ana uwezo wa kujionesha mwenyewe na kutangaza kazi pamoja na mafanikio yake.
Miriam Odemba amekuwa akifanya kazi za uanamitindo katika majukwaa ya kimataifa na amewahi kushiriki mashindano mbalimbali ya urembo, akijijengea historia katika tasnia hiyo.
Kauli yake imeibua mjadala kuhusu nafasi ya kujitangaza katika kujenga jina na taaluma, pamoja na namna mafanikio ya watu mbalimbali yanavyoweza kutambuliwa bila kuonekana kama yanashindana.




