Warembo 15 kuwania taji la Miss Temeke 2026

DAR ES SALAAM: WAREMBO 15 wanatarajiwa kushindania taji la Miss Temeke 2026, huku washiriki watano watakaofanya vizuri wakipata nafasi ya kuiwakilisha wilaya hiyo katika mashindano ya Miss Dar es Salaam yanayotarajiwa kufanyika Novemba 12, mwaka huu.
Fainali za Miss Temeke 2026 zimepangwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu, katika Ukumbi wa Mbaruku Mwandoro, viwanja vya Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mratibu wa mashindano hayo, Michael Maurus, amesema mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kuwatambulisha warembo kwa Watanzania, kueleza hatua iliyofikiwa katika maandalizi na kuwapa wadau nafasi ya kujitambulisha pamoja na kueleza mchango wao.
Maurus amesema Miss Temeke ni sehemu ya mchakato wa kuelekea mashindano ya Miss Tanzania, ambapo warembo watakaofanya vizuri katika ngazi ya wilaya watapata fursa ya kushiriki Miss Dar es Salaam kabla ya kuendelea na hatua zinazofuata za mashindano hayo.
“Maandalizi ya mwaka huu yana umuhimu wa pekee kutokana na matarajio ya Tanzania kuandaa mashindano ya Miss World mwakani, hivyo kuwataka wadau kushirikiana katika kukuza vipaji na kuwaandaa warembo wenye uwezo wa kuiwakilisha nchi katika majukwaa mbalimbali.
Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Miss Temeke 2026, Halima Rajabu, amesema warembo hao wanatarajiwa kuanza mazoezi wiki ijayo, huku wakishiriki shughuli za kijamii ikiwemo usafi wa mazingira na upandaji miti.
Amesema washiriki pia watapatiwa semina maalumu zitakazolenga kuwajengea uwezo kiakili, kimaadili, kiafya na kijamii, ili kuwaandaa kuwa wanawake wanaojiamini, wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya jamii na kuwa viongozi wa baadaye.
Naye Meneja wa Urban Stay Hotel, Chilongawi Julias, amesema hoteli hiyo imeamua kudhamini mashindano hayo kutokana na mchango wake katika kuibua vipaji, kujenga nidhamu na kuimarisha uwezo wa vijana wa kike.
Julias amesisitiza kuwa urembo haupaswi kutazamwa kwa mwonekano wa nje pekee, bali pia unapaswa kuwa jukwaa la kuwawezesha wasichana kujiamini, kukuza vipaji vyao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Mashindano ya Miss Temeke 2026 yanatarajiwa kuwa fursa kwa warembo hao kuonesha vipaji na uwezo wao, huku yakilenga kuendeleza safari yao katika mashindano ya urembo kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa.




