Ndumbaro mgeni rasmi Ladies First

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa mashindano ya Riadha ya wanawake (Ladies First) msimu wa sita yanaanza Ijumaa, Novemba 22 hadi 24, kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, jijini.
Katibu Mtendaji wa Bazara la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha amesema mashindano hayo yatashirikisha wanariadha 155 na viongozi kutoka mikoa 31 Tanzania Bara na visiwani Zanzibar.
Amesema wataendesha semina kuhusu masuala ya wanawake na mafunzo Kwa makocha itafanyika siku mashindano yatapofanyika.
“Katika ufunguzi tunatarajia mgeni rasmi awe Waziri Ndumbaro kuanza michezo yetu, hafla ya ufunguzi itaambatana na matukio yakiwemo mazoezi ya viungo na mbio za pole yatashirikisha wanajogging 500 wa Temeke,” amesema.
Neema amesema msimu huu utakuwa tofauti na awali, safari hii wamezingatia umri wa wasichana wakiwa na umri chini ya miaka 20 kwa lengo la kuibua vipaji.
“Washiriki watashindana mbio za mita 100, 200, 400, 1500, 5000, 10000,4×100 kwa kupokezena vijiti na kurusha mkuki.
Naye mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Kimatifa la Japani, Ara Hitoshi amesema lengo ni kuimarisha ushiriki wa wanawake katika michezo.
Amesema mashindano hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kutoa fursa kwa wasichana na kuchochea usawa wa kijinsia katika michezo.
“Umuhimu wa tukio hili unazidi mashindano au ushindani, linaakisi usawa wa kijinsia,uwekezaji wa wanawake na uhamasishaji wa michezo na kuendeleza elimu ya viungo ,” amesema.