Nyumbani

Mzee Onyango afariki dunia

DAR ES SALAAM:TASNIA ya filamu nchini imepata pigo kufuatia kifo cha mwigizaji mkongwe, Issa Joseph maarufu kama Mzee Onyango, ambaye amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, Juni 11, 2026.

Mzee Onyango amefariki katika Hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua kwa muda.

Akizungumza na waandishi wa habari, mtoto wa marehemu, Joshua Joseph Issa, amesema baba yake alifariki majira ya saa 8 usiku akiwa hospitalini hapo.

Ameeleza kuwa familia imepokea msiba huo kwa huzuni kubwa na kwa sasa inaendelea na vikao vya maandalizi ya mazishi.

Msiba wa marehemu upo eneo la Kawe, jirani na Viwanja vya Gofu vya Lugalo, jijini Dar es Salaam, ambapo ndugu, jamaa na marafiki wanaendelea kufika kutoa pole kwa familia.

Joshua ameongeza kuwa taarifa rasmi kuhusu ratiba na taratibu za mazishi zitatolewa baadaye mara baada ya familia kukamilisha maandalizi muhimu.

Kwa upande wake, rafiki wa karibu wa marehemu na mwigizaji mwenzake wa muda mrefu, Mahamood Marijebi maarufu kama Mwita Mwaranya, amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mzee Onyango, akimtaja kuwa mmoja wa wasanii waliotoa mchango mkubwa katika ukuaji wa tasnia ya filamu nchini.

Kifo cha Mzee Onyango kinaacha pengo kubwa katika sekta ya sanaa na burudani, ambapo atakumbukwa kwa kazi zake mbalimbali zilizogusa maisha ya Watanzania wengi kwa miaka mingi.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button