Nyumbani

Mzamiru, Ngoma wampasua kichwa Kagoma

ISMAILIA: KIUNGO Mkabaji wa Simba, Yusuph Kagoma ni kama ametangaza hali ya hatari kwa namba ndani ya kikosi cha timu hiyo kwa kudai anapambana kumshawishi kocha Fadlu Davids kupata kikosi cha kwanza.

Amekiri kuwepo na ushindani mkubwa wa namba ndani ya timu hiyo kutokana na wachezaji waliopo kwenye kikosi cha timu hiyo kwa msimu wa 2024/25 wa mashindano yaliyopo mbele yao ikiwemo Ligi Kuu Tanzania na kombe la Shirikisho Afrika .

Kagoma anakutana na ugumu wa namba na wachezaji wenzake akiwemo Debora Fernandes na Augustine Okejepha ambao  ni usajili mpya wako katika wakati mgumu wa kuweza kuwapokonya namba Mzamiru Yassin na Fabrice Ngoma waliopo tangu msimu uliopita.

Kiungo huyo amesema anatakiwa kupambana mazoezini kutafuta nafasi ndani ya kikosi cha kwanza kwa kujituma na kufuata maelekezo anayopewa na benchi la ufundi linaloongozwa na Fadlu.

“Suala la kugombea namba lipo kila timu na hilo halinipi shida, nitapambana kulishawishi benchi la ufundi kunipa nafasi, msimu huu naamini tutafanya vizuri kwa sababu ya ubora na uimara wa kikosi tulichonacho.

Ushindani huwezi kuukwepa kutokana na kuhusisha wachezaji wengi bora, binafsi siogopi ushundani wa namba nipo kwa ajili ya kupambana na kujitoa kwenye timu kufikia malengo,” amesema Kagoma.

Ameongeza kuwa anafahamu mashabiki wa Simba wana matumaini makubwa kwa msimu mpya na wamejipanga kuhakikisha wanawapa furaha kwa kufikia malengo ikiwemo kurejesha mataji ndani ya klabu hiyo.

Related Articles

Back to top button