Mwanafa: Stars nendeni mkapambane

TANGA: NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma ‘Mwanafa’ ameitakia kila la heri timu ya soka ya taifa ‘Taifa Stars’ na kuwataka kwenda kupambana na kushinda katika mchezo ujao wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Morocco.
Taifa Stars inatarajia kucheza na Morocco Machi 26, mwaka huu ugenini nchini Morocco. Tayari Stars wameondoka Leo kuelekea huko kwa ajili ya mchezo huo.
Akizungumza mkoani Tanga kwenye hafla ya futari ya kuwaaga Stars, Mwanafa amesema anawatia moyo na kuwaombea kwa Mungu ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
” Ninyi ndugu zetu mmeshaonesha jinsi matokeo yalikuwa hayaonekani ya nakuja upande wetu na yakatokea, siamini kama hili liko nje ya uwezo wenu, mnafahamu kila kitu sisi wengine hatujui,
“Lakini mkiweka mioyo yenu na mkiwa na dhamira ya dhati ya kutaka kushinda mechi hii mtakwenda kushinda, mnakwenda vitani, sisi tunawaamini nendeni mkapambane tuko nyuma yenu,”amesema.
Amesema kwa sasa hawana cha kuahidi lakini timu hiyo ikishinda watapata nguvu ya kuongea na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya chochote kitu kama ilivyo kawaida.
Katika kundi E kinara ni Morocco yenye pointi tisa, ikifuatiwa na Niger sita sawa na Tanzania katika nafasi ya tatu, Zambia nafasi ya nne kwa pointi tatu huku Congo na Eritrea zikiwa hazina pointi.