Simba yamuita Mwamposa kwa Mkapa

DAR ES SALAAM: KATIKA kuendelea kuongeza morali na hamasa kwa mashabiki kuelekea mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry ya Misri, klabu ya Simba imetangaza kuwa Mtume Maumee Boniface Mwamposa, maarufu kama Buldoza, atakuwa miongoni mwa wageni maalum katika mchezo huo mkubwa.
Mtume Mwamposa ataungana na wageni maalum wengine waliotangazwa awali, wakiwemo Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora tayari amekubali mwaliko na kupanga ratiba zake ili kuweza kushuhudia mechi hiyo muhimu ambayo itaamua nani anaingia hatua ya nusu fainali.
“Safari hii tumedhamiria, Ubaya Ubwela! Tunamualika kila mtu mwenye mchango mkubwa kwenye jamii hii. Wachawi ni wengi ndugu zangu, kuna watu wamekunja nafsi kwelikweli,” alisema Ahmed kwa msisitizo.
Kwa mantiki hiyo, Simba wameamua kumualika pia Mtume Mwamposa kama mgeni maalum, huku mazungumzo yakiendelea ili hata waumini wake waweze kununua tiketi mapema na kujitokeza kwa wingi uwanjani.
Ahmed pia alibainisha kuwa timu ya Al Masry inatarajiwa kuwasili nchini Jumapili, Aprili 6, tayari kwa mchezo huo wa marudiano utakaopigwa Jumatano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.